IQNA

Mufti wa Saudia; Si sahihi kususia bidhaa za Magharibi!

13:39 - January 26, 2009
Habari ID: 1736039
Mufti wa Saudi Arabia ametoa matamshi ya kustaajabisha akiwakosoa watu wanaosusia bidhaa za nchi za Magharibi nchini humo kwa sababu ya kuwaunga mkono wananchi wanaokandamizwa na Wapalestina na kupinga uungaji mkono wa nchi za Magharibi dhidi ya jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza.
Sheikh Abdulaziz Aal Sheikh amesema, inajuzu kubadilishana biashara kati ya nchi mbalimbali na si sahihi kususia biadhaa za nchi za Magharibi.
Mufti huyo wa Saudi Arabia ameendelea kujikomba kwa mabeberu wa kimataifa katika hotuba yake ya hivi karibuni kwenye Chuo Kikuu cha Imam Turki bin Abdullah mjini Riyadh akisema kuwa watu wanaosusia bidhaa za nchi za Magharibi ni watu wasiokuwa thabiti katika itikadi zao.
Sheikh Aal Sheikh amesema: Dunia ya leo ni mithili ya mnyororo mmoja na hakuna nchi inayoweza kujitosheleza na kwamba kususia bidhaa za Wamagharibi hakutasaidia lolote.
Mufti wa Saudi Arabia aliyasema hayo kufuatia wito unaotolewa na wanazuoni na jumuiya mbalimbali za kidini na kisiasa zinazohimiza juu ya kususiwa bidhaa za utawala haramu wa Israel na nchi za Magharibi hususan Marekani kwa sababu ya jinai na mauaji ya kikatili ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Gaza.
Nchi nyingi za Kiislamu na Kiarabu pia tayari zimeanza kususia bidhaa za nchi za Magharibi hususan Marekani. 353789
captcha