Balozi huyo wa Jordan anarejea Tel Aviv, makao ya kisiasa ya utawala wa Kizayuni, katika hali ambayo damu ya maelfu ya Wapalestina waliouawa na kujeruhiwa katika hujuma ya Wazayuni Ghaza bado haijakauka.
Kwa mujibu wa mtandao wa Arab online, Ali al-Ayed aliitwa nyumbani siku moja baada ya kuanza hujuma ya kinyama ya Israel huko Gaza. Mfalme wa Jordan aliamua kumuita nyumbani balozi huyo kufuatia malalamiko ya watu wa nchi hiyo.
Wakuu wa Jordan wametoa kisingizo kuwa balozi huyo amerejea Tel Aviv eti kwa ajili ya kurahisisha njia za kutuma misaada ya kibinadamu ya nchi za Kiarabu kwa watu wa Gaza.
Baadhi ya vyama vya kisiasa vya Jordan vimelaani vikali hatua ya serikali ya Amman kumrejesha balozi huyo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Aidha wametaka balozi wa Utawala wa Kizayuni afukuzwe nchini Jordan kama njia ya kulalamikia jinai za utawala huo dhidi ya watu wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza.
Itakumbukwa kuwa katika siku zote 22 za uvamizi wa kinyama wa Israel huko Gaza, Mfalme wa Jordan pamoja na mwenzake wa Saudi Arabia na Rais wa Misri walinyamaza kimya na hata walikuwa na vikao vya siri na wakuu wa utawala wa Kizayuni. Watawala hao watatu wa Kiarabu pia waliunga mkono kwa njia moja au nyingine hujuma ya Wazayuni huko Gaza lengo likiwa ni kuhakikisha harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imeangamizwa. 355028