Kwa mujibu wa gazeti la Al Watan la Saudi Arabia, kikao hicho cha kimataifa kinafanyika chini ya usimamizi wa Mfalme Abdullah bin Abdulaziz wa Saudi Arabia na kitahudhuriwa na wanasiasa maarufu kutoka sehemu zote duniani pamoja na wawakilishi wa dini za mbinguni za Kiislamu, Kiyahudi na Kikristo.
Washriki katika kikao hicho watajadili njia za kuimarisha ushirikiano na mshikamano baina ya wafuasi wa dini na tamaduni mbalimbali. Aidha washiriki watajadili njia za kuondoa hitilafu zilizopo baina ya dini mbalimbali na ustawishaji amani na utulivu duniani.
Kati ya malengo mengine ya kikao hicho ni kujadili namna ya kuzuia uvunjiwaji heshima dini na matukufu yake, kuheshimu thamani za tamaduni mbalimbali, kutatua tatizo la Palestina na kupambana na umasikini duniani.
Kikao cha mazungumzo ya dini na staarabu mjini Riyadh ni katika mkakati wa kufuatilia vikao vya mazungumzo ya dini vilivyofanyika Madrid Uhispani na New York Marekani mwaka 2008. 357277