IQNA

Mapinduzi ya Kiislamu yaimarisha moyo wa mapambano ulimwenguni

10:42 - February 07, 2009
Habari ID: 1741061
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliimarisha moyo wa kujitegemea na kujiamini katika mataifa yaliyokuwa yakipigania uhuru ulimwenguni na kuyafundisha makundi ya mapambano kwamba, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kujiamini pamoja na kuzingatia umoja, yanaweza kuwashinda madhalimu na madikteta duniani.
Hayo yamesemwa na Ali Muhammad Helmi, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uingereza. Bwana Helmi amesisitiza kwamba, kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, hakuna nchi yoyote ulimwenguni iliyokuwa ikidhani kwamba kulikuwepo uwezekano wa kuanzisha harakati za mapambano na hatimaye kushinda bila ya kuyategemea mataifa yenye nguvu kubwa ya Magharibi na hasa Marekani, lakini Mapinduzi ya Kiislamu yalikadhibisha fikra hiyo na kuwathibitishia walimwengu kwamba, jambo hilo linawezekana kabisa.
Ali Muhammad Helmi amesema, kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo hayakutegemea kambi ya Magharibi iliyokuwa ikiongozwa na Marekani wala Mashariki iliyokuwa ikiongozwa na Muungano wa Sovieti ya zamani, kambi mbili zote ambazo zilikuwa zikimuunga mkono dhalimu Shah wa Iran, fikra hiyo ilivunjwa na kusajiliwa katika historia. Amesema, Iran ya Kiislamu iliweza kutoa mfano bora zaidi wa taifa kujitegemea na kujiamini na hivyo kuhuisha moyo wa mapambano na kujiamini miongoni mwa mataifa mbalimbali yaliyokuwa yakipigania uhuru duniani.
Amesema mfano bora zaidi wa hali hiyo unaonekana huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, ambapo Wapalestina kwa kuendesha mapambano yao ya muda mrefu dhidi ya ukandamizaji na jinai za utawala huo, hii leo wamegeuka na kuwa nguvu kubwa isiyoweza kushindwa na jeshi la utawala huo ambalo limejizatiti kikamilifu kwa silaha za kisasa kabisa.
Huku akiashiria kwamba Mapinduzi ya Kiislamu yalitofautiana sana na mapinduzi mengine yaliyotokea katika pembe mbalimbali za dunia yakiwemo ya Ufaransa na Russia, ambayo kimsingi yalikuwa yakitegemea sana masuala ya kimaada na ya kidunia tu, Bwana Helmi amesema kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu yalitegemea sana thamani za Kiungu na kimaanawi. Amesema, jambo hilo limeyapa Mapinduzi ya Kiislamu uwezo mkubwa na kuyafanya yazingatiwe ulimwenguni kama nguvu kubwa ya kieneo na kimataifa.
Bwana Helmi ameashiria pia mashinikizo na propaganda kubwa zinazotekelezwa na nchi za Magharibi kwa lengo la kuishinikiza Iran iwachane na misingi yake ya Kiislamu kwa kudai kwamba masuala ya kidini hayaoani na mahitaji ya mwanadamu wa leo na akasema kuwa umri wa Mapinduzi ya Kiislamu na maendeleo makubwa ambayo yamepatikana katika kila nyanja kutokana na mfumo huo ni ushahidi wa kutosha kwamba mfumo huu wa Kiislamu unadhamini mahitaji yote ya mwanadamu ya hapa duniani na huko Akhera. 358842
captcha