IQNA

Wafaransa wataka miamala ya Kiislamu itumike nchini humo

18:51 - February 12, 2009
Habari ID: 1743235
Wataalamu wa masuala ya kifedha wa Ufaransa wamefanya kikao chini ya anwani 'Upeo wa Kunufaika na Miamala ya kifedha ya Kiislamu barani Ulaya' huko mjini Paris na kutaka Wafaransa wanufaike na miamala ya Kiislamu na kuimarishwa huduma za kifedha za Kiislamu nchini humo.
Wataalamu wa masuala ya kifedha wa Ufaransa wameitaka serikali ya nchi hiyo kutonufaika tu na uzoefu wa uwekezaji wa benki za Kiislamu bali kutekeleza na kukubali miamala ya Kiislamu. Wamesisitiza kwamba, moja ya njia za kukabiliana na mzozo wa kifedha unaoukabili ulimwengu wa Magharibi hivi sasa ni kunufaika na huduma za kifedha kwa msingi wa sheria za Kiislamu. Wameitaka serikali ya Paris kuziruhusu benki za nchi hiyo kutekeleza mfumo wa kifedha wa Kiislamu katika utoaji wa huduma zao kwa raia wa nchi hiyo.
Wataalamu hao wa Ufaransa wamekaribisha msimamo wa Christine Lagarde, Waziri wa Uchumi wa nchi hiyo wa kuondoa marufuku ya sheria na kodi ya nchi hiyo kuhusiana na kuchapishwa sarafu za Kiislamu nchini humo.
Kikoa hicho pia kimesisitiza kwamba, serikali ya Ufaransa inaweza kuanzisha benki za Kiislamu na kutoa huduma za kifedha kwa msingi wa sheria za Kiislamu na hivyo kuweza kunufaika na uwekezaji mkubwa wa matajiri wa Kiislamu na kustawisha haraka uchumi wa Ufaransa. Wataalamu hao wamesema mwishoni mwa kikao hicho kwamba, juhudi zilizofanywa hadi sasa hazitoshi kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya Waislamu wa nchi hiyo ambayo ni karibu Waislamu milioni 6, kwa sababu Waislamu hao wanataka kuwekeza katika miradi ya kifedha ya nchi hiyo isiyotoa riba na inayokwenda sambamba na sheria za Kiislamu. 362586
captcha