Kanisa la Antakia la mjini Damascus Syria, limetoa taarifa likilaani dharau ya waendeshaji wa kipindi cha tamthilia chekesha au futuhi katika televisheni moja ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Nabii Issa na mama yake mtakatifu (as).
Kwa mujibu wa shirika la habari la Syria Sana, wakuu wa kanisa hilo wameyataja matamshi yaliyotolewa na waendeshaji wa kipindi hicho dhidi ya Nabii Issa na mama yake mtakatifu (as) kuwa ni uzushi na uongo mtupu na kwamba yanatokana na hisia zao za kibaguzi na zilizo dhidi ya ubinadamu. Wamesema, kutangazwa hewani kipindi kama hicho na wawakilishi wa watu waliomsulubu Nabii Issa (as) si jambo la kushangaza.
Taarifa hiyo imewataka wapigania haki wote duniani kulaani kwa maneno makali dharau hiyo ambayo imesema ni dharau kwa matukufu ya dini zote za mbinguni na tauhidi.
Vilevile viongozi wa Kikristo wa Syria wametoa taarifa wakilaani vikali dharau hiyo dhidi ya Mtukufu Issa (as) katika televisheni ya utawala haramu wa Israel na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya waendeshaji wa kipindi hicho kilichokanyaga matukufu ya kidini. 369761