IQNA

Misikiti ni ngome ya mapambano dhidi ya hujuma ya kiutamaduni

12:38 - March 04, 2009
Habari ID: 1751358
Misikiti ni ngome muhimu ya kupambana na hujuma ya kiutamaduni ya nchi za Magharibi kwa sababu tukikaa kimya dhidi ya hujuma hiyo ya maadui tutakabiliwa na pigo kubwa.
Hayo yamesemwa na Ridha Jadidi, Mshauri wa Meya na ambaye pia ni mkuu wa idara inayosimamia maswala ya usimamishaji swala katika mkoa wa Isfahan nchini Iran. Amesema, Mapinduzi ya Kiislamu yalileta mafanikio na baraka nyingi zikiwemo za kuzidishwa ujenzi wa misikiti na vituo vya utamaduni nchini, vituo ambavyo vimekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha shughuli za sanaa, fasihi, masuala ya kijamii na kisiasa.
Akisisitiza kwamba Uislamu ni dini ya kijamii, Ridha Jadidi amesema kuwa kukusanyika vijana kwenye misikiti kunapelekea vijana hao kuimarika kifikra, kiutamaduni na kifasihi. Amesisitiza umuhimu wa kuwepo uhusiano imara kati ya familia mbalimbali na misikiti na kuongeza kuwa, kuanzishwa kwa maktaba katika misikiti ni njia bora zaidi ya kuimarisha utamaduni kwa maslahi ya jamii nzima ya Kiislamu.
Ridha Jadidi amesema kuwa misikiti ni ngome muhimu ya kupambana na hujuma ya kiutamaduni ya maadui na kwamba hatua za lazima zisipochukuliwa kuhusiana na suala hilo basi jamii ya Kiislamu itakabiliwa na pigo kubwa la kiutamaduni kutoka kwa maadui hao. Amesema, hii ni kutokana na ukweli kwamba daima maadui wa ndani na nje ya mipaka ya Iran wanapanga mipango ya kufikia malengo yao machafu na hatari dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesisitiza kwamba hata kama vita vya utamaduni havionekani kwa macho lakini athari zake ni haribifu mno katika jamii. 372181
captcha