IQNA

Malalamiko ya maulama wa Misri dhidi ya pendekezo la kubadilishwa vitabu vya Kiislamu

12:47 - March 05, 2009
Habari ID: 1752027
Mapatano ya chuo kikuu cha kidini cha al-Azhar na Vatican kwa lengo la kubadilishwa vitabu vya masomo vya wanafunzi kwa lengo la kuondoa humo kile kinachotajwa kuwa ni dharau kwa wafuasi wa dini yamezusha malalamiko makubwa ya wanazuoani wa Misri.
Wanazuoni hao wanasema kuwa hakuna haja ya kutazamwa upya vitabu vya masomo vya wanafunzi wa Misri kwa sababu vitabu vya Waislamu haviruhusu kufanyiwa dharau wafuasi wa dini nyinginezo.
Wanazuoni hao wamesisitiza kwamba tatizo kuu linapatikana katika vitabu vya nchi za Magharibi ambazo daima hufanya juhudi za kutusi na kuukosea heshima Uislamu, Manabii na Mtume Muhammad (saw). Kwa msingi huo, wanasisitiza kwamba vitabu vya masomo vya nchi hizo ndivyo vinavyopasa kufanyiwa marekebisho ya kimsingi.
Wahadhiri kadhaa wa chuo cha al-Azhar wamesema kuwa Muhammad Tantawi, mkuu wa chuo hicho alitoa amri ya kutazamwa upya vitabu hivyo siku nyingi zilizopita na kwamba hivi sasa hakuna jambo lolote linaloshukiwa katika vitabu hivyo.
Kuhusiana na suala hilo Taha Rayan, mmoja wa wahadhiri wa chuo hicho anasema kuwa vitabu vya masomo vya Waislamu havina haja ya kufanyiwa marekebisho kwa sababu dini tukufu ya Kiislamu inawasihi wafuasi wake kuheshimu wafuasi wa dini nyinginezo.
Siku chache zilizopita washiriki wa kikao cha pamoja cha al-Azhar na Vatican walitaka kufutwa katika vitabu vya masomo mambo yanaoonekana kuwa ni dharau kwa wafuasi wa dini. 372825
captcha