IQNA

Kumalizika kikao cha kuwaunga mkono Wapalestina mjini Tehran

17:36 - March 07, 2009
Habari ID: 1752910
Kikao cha Nne cha Kimataifa cha 'Uungaji mkono kwa Taifa la Palestina, Dhihirisho la Mapambano; Gaza Mhanga wa Jinai' kilimalizika siku ya Ijumaa Tarehe 6 Machi hapa mjini Tehran kwa hotuba ya Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu au Bunge la Iran.
Kikao hicho cha siku mbili kilianza siku ya Jumatano kwa hotuba ya Ayatullahil Udhma Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa ya mwisho ya kikao hicho, Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameashiria mipango ambayo imekuwa ikitekelezwa katika kipindi cha miaka iliyopita eti kwa lengo la kuleta amani katika Mashariki ya Kati na kusema kuwa mipango hiyo yote imefeli na kutofikia natija yoyote kutokana na dhulma ya nchi za Magharibi. Amesema kuwa jambo linalohitajika hivi sasa kwa ajili ya kuleta suluhu ya kudumu katika eneo hilo ni kutekelezwa mipango adilifu na inayozingatia hali halisi katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Akizungumza katika kikao hicho pia, Manuchehr Muttaki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba mara tu baada ya kuingia madarakani serikali halali iliyochaguliwa na wananchi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu Hamas, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na nchi za Ulaya, zilianzisha propaganda sumu dhidi ya serikali hiyo na kutangaza wazi kwamba lengo lao kuu ni kuiangusha serikali hiyo. Amesema propaganda zimekuwa zikienezwa dhidi ya harakati hiyo ya Kiislamu ili kuzima mapambano halali ya wananchi wa Palestina.
Kikao hicho hatimaye kilitoa taarifa, ambapo pamoja na mambo mengine mengi, iliunga mkono mapambano hayo ya taifa la Palestina na kulaani hatua za utawala ghasibu wa Israel za kubadili muundo wa kijamii wa Palestina ambao ni wa Kiislamu na Kiarabu na kuufanya kuwa wa Kiyahudi. 373449
captcha