Kikao cha sita cha utafiti wa Qur'ani ambacho hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili, ambacho mara hii kitafanyika chini ya anwani ya 'Qur'ani, Matini, Historia na Utamaduni' kimepangwa kufanyika tarehe 12 hadi 14 Mwezi Novemba, katika Kitengo cha Utafiti wa Mashariki na Afrika cha Chuo Kikuu cha London.
Kwa mujibu wa tovuti ya kitengo hicho lengo la kufanyika kikao hicho ambacho kimeandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Kiislamu cha Chuo Kikuu cha London ni kuchunguza pande mbalimbali za Qur'ani na kuwasilisha matokeo ya uchunguzi uliofanywa awali kuhusiana na masuala mbalimbali ya Qur'ani. Vilevile historia fupi ya shughuli za kidini, kifikra na kisanaa katika nyanja za Qur'ani itawasilishwa katika kikao hicho.
Kituo cha Utafiti wa Kiislamu cha Chuo Kikuu cha London kimetoa mwaliko kwa watafiti, wachambuzi, wataalamu na wafuatiliaji wa masuala ya Qur'ani kuwasilisha makala fupi za utafiti wao wa Qur'ani hadi kufikia tarehe Mosi Juni. Masuala yaliyopangwa kujadiliwa nayanayotakiwa kutumwa kwa kikao hicho ni pamoja na uchunguzi wa matini ya Qur'ani, nuskha za zamani za Qur'ani, Tafsiri za Qur'ani za zamani na za kisasa, masomo ya dini ya Kiislamu na Qur'ani, sheria za Kiislamu na Qur'ani, irfan na Qur'ani, nadharia za kifalsafa kuhusiana na Qur'ani, Qur'ani katika fasihi za zamani na za kisasa, tarjumi za Qur'ani, sanaa ya Qur'ani na madhehebu, Qur'ani katika utamaduni wa umma, mitazamo ya kibinadamu na kijamii kuhusiana na Qur'ani, Qur'ani katika nyanja za masomo, Qur'ani katika ulimwengu wa sasa na utafiti wa kisasa kuhusiana na Qur'an.
Makala bora zitakazowasilishwa katika kikao hicho yatachapishwa katika jarida la Utafiti wa Qur'ani la Kitengo cha Utafiti wa Qur'ani cha Chuo Kikuu cha London. 375411