IQNA

Maulidi ya Mtume (saw) yafanyika Chechnia

10:12 - March 11, 2009
Habari ID: 1754545
Maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Muhammad (saw) yalifanyika siku ya Jumatatu huko Grozni, mji mkuu wa Chechnia. Kwa mujibu wa shirika la habari la Frans Press, sherehe hizo zilihudhuriwa na Rais Ramadhan Qadirov wa Jamhuri ya Chechnia na Rais Evkourov wa Ingushetia katika eneo la Caucasia Kaskazini.
Waislamu wa Chechnia wapatao 20,000 walishiriki katika sherehe hizo zilizofanyika katika msikiti wa Ijumaa wa Grozni.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Qadirov amesema kuwa katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, kundi la Mawahabi lilikuwa limeeneza satuwa yao katika jamhuri hiyo na kupinga kufanyika sherehe za kuadhimisha maulidi ya Mtume, lakini kufanyika kwa kishindo sherehe hizo katika pembe mbalimbali za jamhuri hiyo ni jambo linalothibitisha kwamba njama za kundi hilo za kudhoofisha mapenzi ya Waislamu kwa Mtume wao zimegonga ukuta. Amesema kuwa jambo hilo linaonyesha wazi kwamba watu waliokuwa na lengo la kuingiza katika Uislamu masuala yanayopingana na misingi ya mafundisho ya Kiislamu wameshindwa kufikia lengo hilo katika jamhuri hiyo.
Rais Qadirov amesema kuwa ugaidi umemalizika kabisa katika jamhuri hiyo na kwamba hakuna mtu wa kuyaunga mkono tena makundi ya kigaidi katika jamhuri hiyo. Ameahidi kutoa msaada wa karibu euro 1000 kwa kila familia ambako mtoto wa kiume atazaliwa katika siku hizi za kuadhimishwa kuzaliwa Mtume Mtukufu (saw). 375863
captcha