Kikao cha tano cha Baraza la Uratibu wa Shughuli za Qur'ani nje ya mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kikiwa na maudhui ya kuratibu mipango ya Qur'ani katika mwaka ujao wa Kiirani wa 1388, na ambacho kimewashirikisha wawakilishi wa taasisi na mashirika mbalimbali ya Qur'ani, kimefanyika kwa uratibu wa Ofisi ya Naibu Mkuu wa Taasisi ya Masuala ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu.
Mahmoud Waidhi, Naibu Mkuu wa Masuala ya Utamaduni na Mawasiliano wa ofisi iliyotajwa amesema kuwa hadi sasa shughuli za Qur'ani ambazo zimefanyika nje ya nchi ni ndogo na chache mno na kwamba juhudi zaidi zinapasa kufanywa kwa ajili ya kuboresha shughuli hizo. Amesema, kuna haja kubwa ya kufanyika kazi za msingi katika uwanja huo na kuepuka shughuli zisizozingatia masuala kwa kina.
Akizungumzia umuhimu wa wahusika wa masuala ya Qur'ani kushirikiana na vitengo vya utamaduni vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kuimarisha shughuli za Qur'ani, Mahmoud Waidhi amesisitiza kwamba juhudi maradufu zinapasa kufanywa kwa ajili ya kuwasilisha shughuli mbalimbali za Qur'ani pamoja na uchapishaji vitabu vinavyohusiana na kitabu hicho kitakatifu katika pembe mbalimbali za dunia ili kuwanufaisha watu kwa thamani kubwa za kielimu, kimafunzo na kimalezi za kitabu hicho. 375665