IQNA

Taarifa ya mwisho ya kikao cha Umoja wa Kiislamu

14:59 - March 17, 2009
Habari ID: 1756737
Wasomi na wanafikra walioshiriki kikao cha kimataifa cha 22 cha Umoja wa Kiislamu wametoa taarifa mwishoni mwa kikao hicho wakilaani vikali kila aina ya uchokozi na uvamizi wa utawala haramu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina.
Pia wamesisitiza kutolewa malezi kwa vizazi vya Kiislamu kwa msingi wa utamaduni, mapambano na utukufu.
Taarifa hiyo imesisitiza juu ya muamko wa Kiislamu miongoni mwa Waislamu kwa lengo la kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu. Imesema, hitilafu ndogondogo za Waislamu hazipasi kuwagawanya kisiasa.
Washiriki wa kikao hicho wamesema kuwa umma wa Kiislamu hivi sasa unakabiliwa na changamoto kubwa ambazo zimewalenga shakhisia na wasomi wa kiutamaduni na kisiasa kwa lengo la kuvuruga ustaarabu wa Kiislamu. Wamesema, njama hizo zimelenga kuubakisha nyuma umma mzima wa Kiislamu katika nyanja za kielimu, kiuchumi na kijeshi na pia kuutenga Uislamu na madaraka na kuwafanya wafuasi wake waige na kufuata kibubusa utamaduni wa nchi za Magharibi.
Taarifa hiyo pia imeelezea masikitiko makubwa ya Waislamu kutokana na mielekeo ya kupindukia mipaka na fikra za kijahili na ujinga zinazoonekana miongoni mwa baadhi ya Wasilamu wasioelewa uhalisi wa mambo na mafundisho sahihi ya dini ya Kiislamu. Washiriki wamesisitiza udharura wa kutekelezwa mipango ya kunyanyua kiwango cha fikra na muamko wa Waislamu na kuhamasisha utekelezwaji wa sheria za Kiislamu.
Kuimarishwa taasisi na mashirika ya pamoja ya Kiislamu, ukiwemo Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC na kunufaika vyema na suhula za kisiasa na kiuchumi za nchi hizo ni miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa katika taarifa hiyo. Imesema matusi na dharau inayofanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Wazayuni dhidi ya Mtume Mtukufu (saw) ni dalili ya wazi ya ujahili na upumbavu wao mkubwa kuhusiana na sifa aali za mtukufu huyo.
Taarifa ya mwisho ya kikao cha Umoja wa Kiislamu imesisitiza kwamba juhudi kubwa zinapasa kufanywa ili kumuarifisha vyema Mtume (saw) katika pembe zote za dunia. Imesema, jambo hilo litasaidia kutambuliwa na kufahamika vyema mtukufu huyo duniani kwamba alikuwa mtu mwema na rehema waliyopewa wanadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwanadamu aliyekamilika katika pande zote na mwenye fadhila na maadili bora ya kibinadamu na ya kupigiwa mfano. 378377
captcha