IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amwambia Obama:

Onyesha kivitendo mabadiliko unayonadi katika kaulimbiu zako

15:28 - March 22, 2009
Habari ID: 1757789
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametoa hotuba muhimu katika hadhara ya umati mkubwa wa watu kwenye Haram ya Imam Ridha (as) mjini Mash'had kaskazini mwa Iran katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia akibainisha nyanja na udharura wa kuwepo maendeleo na uadilifu, sura mbalimbali za marekebisho ya mwenendo wa matumizi, uchaguzi ujao wa Rais nchini Iran na kadhia ya Iran na Marekani.
Khamenei amesema kuwa taifa kubwa na azizi la Iran litatumia muongo wa nne wa Mapinduzi ya Kiislamu kupiga hatua kubwa na harakati ya kufikia malengo yake makuu ya maendeleo na uadilifu, kwa kutilia maanani kuwa tayari kwa taifa hilo na nyanja nyingi chanya zilizopo.
Katika hadhara hiyo kubwa Kiongozi Muadhamu amewapa wananchi wa Iran mkono wa sikukuu ya Nairuzi na mwaka mpya wa Hijria Shamsia na akasema, kuwepo kwa mamilioni ya vijana walioelimika, watanashati na wasomi, uzoefu wenye thamani, watu wenye vipaji maalumu, viongozi na mudiri katika kukabiliana na masuala mbalimbali ya miongo mitatu iliyopita ambako kumetayarisha uwanja wa kuchukuliwa maamuzi muhimu kama utekelezaji wa ibara ya 44 ya Katiba, juhudi kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa wahitaji halisi nchini na safari za viongozi wa serikali katika mikoa na maeneo ya karibu na mbali kote nchini na vile vile kuwa tayari miundo mbinu ya kimsingi katika nyanja mbalimbali za kielimu, kanali za masiliano na uchukuzi ni miongoni mwa mambo ambayo yametayarisha mazingira mazuri kwa ajili ya kupiga hatua za haraka kwa ajili ya kuufanya muongo wa nne wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao ndio umeanza mwaka huu, kuwa muongo wa maendeleo na uadilifu kwa maana halisi ya neno hilo, katika kivuli cha mipango mizuri, uchapakazi na juhudi kubwa.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kwenda sambamba uadilifu na maendeleo na akasema, kupunguzwa mwanya kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi, usawa katika matumizi ya suhula na katika fursa zinazopatikana na kupunguzwa mwanya wa umiliki wa vitu kati ya maeneo tofauti nchini ni miongoni mwa sifa maalumu na za kweli za uadilifu. Ameongeza kuwa, kufanikisha matarajio hayo makubwa ni jambo gumu lakini linalowezekana na inabidi tufanye bidii na juhudi za pamoja kufikia malengo hayo.
Akifafanua vielelezo vya uadilifu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mapambano ya kweli, ya kudumu na yasiyosita dhidi ya ufisadi wa kiuchumi na kijamii na kuongeza kuwa kupatikana maendeleo na uadilifu kunahitajia kuweko viongozi waumini, mashujaa na wenye mipangilio mizuri, wenye iklhasi na azma thabiti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia sisitizo lake kwenye ujumbe wa mwaka mpya wa Nairuzi kuhusu wajibu wa kufanyiwa marekebisho mwenendo wa matumizi na kuongeza kuwa, jambo hilo ni hatua ya kimsingi katika njia ya maendeleo na uadilifu kwani maradhi ya israfu husababisha madhara mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na huhatarisha pia mustakbali wa nchi.
Amesema iktisadi katika matumizi ina maana ya matumizi sahihi, yenye manufaa na yenye kuzaa matunda na kuongeza kuwa, inabidi tukiri kwamba ada, mila na desturi zisizokuwa sahihi zimepelekea watu kuchupa mipaka katika matumizi na kwamba uhusiano baina ya uzalishaji na matumizi umesambaratika kwa madhara ya uzalishaji kiasi kwamba thuluthi ya mikate inayozalishwa na kwa uchache khumusi ya maji yanayotumika vitu ambavyo vinapatikana kwa shida na juhudi kubwa, hupotea vivi hivi. Amesema wastani wa matumizi ya nishati nchini Iran ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa matumizi ya nishati hiyo duniani na inasikitisha kusema kwamba, kiwango cha matumizi ya nishati katika uzalishaji wa bidhaa ni mara nane zaidi ikilinganishwa na nchi zilizoendelea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema marekebisho mwenendo wa matumizi na kujiepusha na israfu ni suala la kidini na kiakili. Amesema, kupambana na israfu na kuwa uangalifu katika matumzi hakuwezekani kwa maneno matupu na kwamba Bunge na Serikali zina wajibu wa kurekebisha mwenendo wa matumizi kuanzisha katika uzalishaji hadi matumizi na utengenezaji upya bidhaa kutokana na vitu viliyotumiwa kwa kuweka sheria sahihi, kuzitekeleza na kufuatilia jambo hilo kwa umakini.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake muhimu aliyoitoa mbele ya mjumuiko mkubwa wa wafanyaziara katika Haram tukufu ya Imam Ridha (as) huko Mash'had, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia suala la uchaguzi wa kumi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema chaguzi ni moja ya nguzo za utawala wa Kiislamu nchini na kuongeza kuwa, demokrasia ya kidini haipatikani kwa maneno matupu bali inahitajia kushiriki, kuwepo na azma thabiti ya wananchi na mfungamano wa kifikra, kiakili na kiroho wa wananchi na mabadiliko ya nchi yao na kwamba hilo haliwezekani ila kwa kufanyika uchaguzi sahihi, na kushirikisha idadi kubwa ya wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, uchaguzi ni uwekezaji na ni akiba muhimu kwa taifa kwa ajili ya uongozi sahihi ya nchi na kuweza kupata mustakbali mzuri taifa. Amesema kila kura inayotumbukizwa katika sanduku la kupigia kura ina umuhimu wake na ina nafasi katika uwekezaji huo wa taifa.
Ayatullah Khamenei amewaambia wagombea katika uchaguzi wa Rais ambao tayari wameshajitokeza na wale watakaojitokeza baadaye kwamba tambueni kuwa uchaguzi si wenzo wa kufikia kwenye madaraka tu bali ni njia ya kunyanyua uwezo wa nchi, kuzidisha ezi ya taifa na kuliletea heshima taifa, hivyo mnapaswa kuzingatia jambo hilo katika mienendo na kampeni zenu na ili mgombea yeyote asije akatumia maneno katika kampeni zake za uchaguzi ambayo yatamtia tamaa adui.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia kadhia ya Iran na Marekani. Amesema tangu awali ya Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa, suala la kuamiliana na Marekani limekuwa mtihani mkubwa kwa taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu. Ameashiria vitendo vya mara kwa mara vya kiadui vya viongozi wa Marekani wawe wa chama cha Republican au cha Democrat dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Iran na akaongeza kuwa, kuwachochea wapinzani na kusaidia vitendo vya uharibifu na kigaidi ni mambo ya kwanza yaliyofanywa na Wamarekani kuonyesha uadui wao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kwamba kwa mujibu wa taarifa sahihi zisizo na chembe ya shaka hadi hivi sasa siasa hizo za kiadui za Marekani zinaendelea kupitia vibaraka wa nchi hiyo na watu waovu katika mipaka ya Iran na Pakistan.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuzuia na kukataa kutoa mabilioni ya dola pamoja na kukacha kulipatia taifa la Iran mali na bidhaa zake, kumshawishi Saddam Hussein aishambulie Iran na baadaye kuunga mkono utawala wake katika vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu ambavyo Iran ililazimishwa kupigana na kupelekea kuuawa shahidi karibu vijana laki tatu wa nchi hii, na jinai ya Marekani ya kuishambulia kwa kombora ndege ya abiria ya Iran katika mwaka wa mwisho wa vita hivyo na kupelekea kuuawa kwa umati watu karibu 300 wanawake, wanaume na watoto wadogo ni miongoni mwa vitendo vya kiadui vya Marekani dhidi ya taifa la Iran na kuhoji kwa kusema: "Je, taifa la Iran linaweza kusahau mambo hayo?"
Vilevile ameashiria vikwazo vya miaka 30 dhidi ya taifa la Iran na uungaji mkono wa Washington kwa magaidi watenda jinai ambao wameuwa watu wengi nchini Iran na kuleta matatizo mbalimbali katika eneo, uungaji mkono usio na mipaka wala masharti wa Marekani kwa Wazayuni watenda jinai na vitisho vya mara kwa mara vya Washington kuwa itaishambulia kijeshi Iran na kuongeza kuwa suala hilo ni miongoni mwa ushahidi wa uadui usio na mwisho wa Marekani dhidi ya taifa la Iran na kusisitiza kwamba, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, wakuu wa Marekani wamewavunjia heshima viongozi wa Iran mara chungu nzima na hata baadhi ya viongozi wa Marekani wanataka taifa hili kubwa lililo na historia iliyojaa fakhari, liangamizwe kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia suala la kuchukua madaraka Rais na serikali mpya nchini Marekani na kuongeza kuwa, hata katika huo ujumbe wa pongezi uliotolewa na Rais wa Marekani kwa ajili ya taifa la Iran kwa mnasaba wa sikukuu ya mwaka mpya Nairuzi, imedaiwa ndani yake kwamba taifa la Iran linaunga mkono ugaidi na linataka kumiliki silaha za nyukli. Amehoji kwamba: "Je, huko ni kutoa mkono wa pongezi au ni kuendeleza tuhuma zilezile za huko nyuma?"
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, hatujui ni nani anayechukua maamuzi huo Marekani. Je ni Rais, au ni Congress au ni watu walio nyuma ya pazia, lakini pamoja na hayo tunasisitiza kwamba wananchi wa Iran ni watu wanaotumia busara na kufanya mambo yao kwa mahesabu na si kwa hamasa jazba.
Akiashiria kadhia ya mazungumzo na kaulimbiu ya Rais mpya wa Marekani yaani mabadiliko, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Kama kuna kitu chochote kilichobadilika ukitoa sehemu ndogo ya lugha mnayotumia kuhusu Iran basi tuonyesheni mabadiliko hayo. Je, uadui wenu dhidi ya taifa la Iran umeisha? Je mumelirejeshea taifa la Iran mali zake? Je vikwazo vyenu dhidi ya taifa hili mumeshaviondoa? Je mumeachana na kueneza uvumi wa uongo na propaganda mbaya dhidi ya taifa la Iran? Je, mumeacha kuulinda na kuunga mkono bila masharti wala mipaka utawala wa Kizayuni wa Israel?
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, mabadiliko hayapaswi kuwa ya maneno matupu au yenye nia mbaya na kama mnachotaka ni kuendeleza malengo yale yale ya huko nyuma kupitia ujanja wa kubadilisha siasa na mbinu zenu hilo bila ya shaka litakuwa ni hadaa na wala si mabadiliko na iwapo kweli mna nia ya kufanya mabadiliko basi inabidi mabadiliko hayo yaonekane katika matendo na vilevile inabidi viongozi wote wa Marekani walijue vyema hili kwamba haiwezekani kulihadaa taifa la Iran.
Aidha amesema viongozi wa Marekani hawana njia nyingine ila kufanya mabadiliko nchini mwao na kuongeza kuwa, kama hamtabadilika jueni kuwa suna ya Mwenyezi Mungu na mataifa mengine duniani yatakubadilisheni.
Akitoa nasaha kwa viongozi wa Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema miongoni mwa sababu zinazopelekea walimwengu waichukie Marekani ni kuendelea nchi hiyo na siasa zake za kibeberu, juhudi zake za kutaka kuwatwisha wengine siasa na matakwa yake na kuamiliana kwake na masuala mbalimbali ya dunia kwa njia ya kindumakuwili. Amewaambia viongozi wa Marekani kwamba: jifunzeni kutokana na matukio hayo, hilo ni kwa maslahi na faida yenu na ya nchi yenu. Achaneni na siasa hizi, mkifanya hivyo sura yenu itaanza kubadilika polepole katika fikra za walio wengi duniani.
Ameongeza kuwa, yatieni akilini na kuyazingatia vizuri maneno yangu haya, na msiwape Wazayuni wakufasirieni, bali shaurianeni na watu wema.
Mwishoni mwa maudhui hiyo amesema, tunachosema sisi ni kuwa, madhali serikali ya Marekani haitabadilisha mbinu, siasa na hatua zake za kiadui za miaka 30 iliyopita dhidi ya taifa letu, basi ijue kuwa taifa la Iran ni lile lile taifa la miaka 30 iliyopita bali linazidi kuwa imara siku baada ya siku na linazidi kupata uzoefu kadiri siku zinavyosonga mbele.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, taifa letu halifurahishwi na lugha ya vitisho na za kutia tamaa. Amesema: "Sisi hatuna historia ya Rais na serikali mpya ya Marekani hivyo tunachoweza kufanya ni kuamiliana nao kulingana na matendo yao.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameelezea kusikitishwa mno na habari ya kufariki dunia mke mpendwa wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) na ametoa mkono wa pole kwa taifa la Iran na kwa wafiwa wote na kuongeza kuwa, shahksia huyo mkubwa alisimama kidete pamoja na Imam katika shida na matatizo yote na amemuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amfufue Imam na mkewe mpendwa na watoto wao pamoja na mawalii wa Mwenyezi Mungu na alijaalie taifa la Iran siku zote liendelee kutukuza na kujua thamani ya Imam Khomeini MA.
Kabla ya hotuba hiyo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Waidh Tabasi mwakilishi wa Fakihi Mtawala katika mkoa wa Khurasan ambaye pia ni msimamizi wa Haram ya Imam Ridha AS alipata fursa ya kuhutubia na kuitumia fursa hiyo kutoka mkono wa baraka kwa mnasaba wa sikukuu ya Nairuzi na kusema kuwa kupewa mwaka huu jina la Mwaka wa Marekabisho ya Mwenendo wa Matumizi ni fursa nzuri ya kutia kasi harakati za kueleka kwenye kufanikisha malengo ya miaka 20 ya maendeleo nchini. 380005
captcha