IQNA

Umma wa Kiislamu unapinga hukumu ya mahakama ya ICC dhidi ya al Bashir

17:07 - March 26, 2009
Habari ID: 1758113
Harakati ya Kiislamu ya Jordan imesema kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya Rais Omar al Bashir wa Sudan ni njama mpya dhidi ya umma wa Kiislamu na kusisitiza kuwa Umma wa Kiislamu umeafikiana kupinga uamuzi huo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kundi la wabunge wa harakati ya A'mal al Islami ya Jordan na kuongeza kuwa harakati hiyo imeshangazwa na matamshi ya Waziri wa Habari wa Jordan aliyesema kuwa iwapo Rais Omar al Bashir atawasili nchini humo atatiwa mbaroni.
Hamza Mansur amesema kuwa matamshi hayo ya Waziri wa Habari wa Jordan hususan katika kipindi hiki nyeti, yanapingwa na Waislamu wote hususan ikitiliwa maanani kwamba umma mzima wa Kiislamu umeafikiana kupinga hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Amesema kuwa uamuzi wa mahakama hiyo dhidi ya Rais wa Sudan ni njama dhidi ya umma wa Kiislamu na kwamba nchi za Kiarabu na Kiislamu zinafanya juhudi za kufutwa uamuzi huo.
Hamza Mansur amesema kuwa matamshi ya Waziri wa Habari wa Jordan yatazusha mgawanyiko kuhusu kadhia hiyo na kwamba serikali ya Amman inapaswa kuweka wazi msimamo wake katika kadhia hiyo.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetoa hukumu ya kutiwa nguvuni Rais Omar al Bashir wa Sudan kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita katika jimbo la Darfur. 380264
captcha