Huku akiashiria umashuhuri wa Mustafa Ismail katika usomaji wa Qur'ani Tukufu, mmoja wa shakhsia muhimu katika uwanja huo amemsifu sana msomaji huyo muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kwamba, alianzisha mbinu mpya katika lahani za usomaji Qur'ani na hivyo kufuatwa na wasomaji wengi katika uwanja huo.
Akizungumzia suala hilo, Abdu ar-Rasuul Ibadi, ustadh mashuhuri wa taaluma ya Qur'ani amechambua mbinu mbalimbali za usomaji Qur'ani zilizotumiwa na Mustafa Ismail na kusema kuwa alipewa kipawa kikubwa cha kusoma Qur'ani kwa mujibu wa maana ya aya zake na hivyo kumfanya msikilizaji kupata taswira tofauti kwenye fikra wakati anaposikiliza usomaji wake. Amesema mara nyingine alikuwa akisimama kwa namna fulani kwenye usomaji wa aya, jambo ambalo lilimvutia msikilizaji kwa njia maalumu.
Amesisitiza kuwa jambo hilo ndilo lililompa umashuhuri mkubwa na kumtofautisha kabisa na wasomaji wengine wa Qur'ani. Amesema, hadi sasa hatujawahi kumpata msomaji mwingine mashuhuri wa Qur'ani aliye na uwezo mkubwa wa kubadili lahani na sauti kuambatana na maana za aya kama alivyokuwa akifanya Mustafa Ismail.
Hata hivyo ustadh Abdu ar-Rasuul amesema kuwa mara nyingine katika kufanya hivyo alikuwa akitoka nje kidogo ya kanuni za tajweedi, jambo ambalo amesema ndilo lililokuwa nukta hasi ya pekee katika usomaji wake kwa sababu lahani haipasi kukiuka misingi ya tajweedi kwa njia yoyote ile. Licha ya hayo, amesema alipewa kipawa kikubwa cha lahani ambayo alikuwa akiitumia vyema katika kuwavutia wasikilizaji wake.
Akijibu swali kuhusu ni kwa nini kuna usomaji mchache sana wa Mustafa Ismail miongoni mwa Waislamu, ustadh huyo wa elimu ya Qur'ani amesema kuwa katika zama za msomaji huyo, hakukuwepo na vinasa-sauti vingi na ndio tukawa tuna uhaba wa usomaji wa msomaji huyo mashuhuri wa Qur'ani katika ulimwengu wa Kiislamu. 374344