IQNA

Qur'ani na Tiba

12:18 - April 06, 2009
Habari ID: 1760962
Dini tukufu ya Kiislamu imesisitiza mno juu ya udharura wa kutafuta elimu na maarifa kwa Waislamu. Tiba ni moja kati ya mambo yaliyozungumziwa katika Qur'ani Tukufu na hadithi. Kutokana na umuhimu wa mitazamo ya Qur'ani kuhusu tiba na afya, hadi sasa kumefanyika vikao na mikutano mbalimbali katika medani ya elimu ya tiba katika mtazamo wa Qur'ani.
Mkutano wa hivi karibuni kabisa kuhusu mada hiyo ni ule uliofanyika tarehe 18 Februari mjini Tehran. Mkutano huo ulihudhuriwa na wasomi wa Qur'ani na madaktari ambao walieleza na kufafanua mitazamo yao kuhusu tiba katika mtazamo wa Qur'ani na hadithi.
Historia inaonyesha kwamba sisitizo la dini ya Kiislamu juu ya udharura wa kutafuta elimu hususan katika uwanja wa matibabu na kutibu wagonjwa liliwahamasisha zaidi Waislamu kutafuta elimu ya tiba tangu zama za awali za kudhihiri dini hiyo. Hali hiyo ilikuwa chachu ya maendeleo makubwa ya kitiba ambayo yalipelekea kudhihiri matabibu hodari kama Abu Ali Sina, Zakaria Razi, Bin Rushd na wengineo ambao wote walitoa huduma kubwa mno kwa ulimwengu wa tiba na utabibu na kuvumbua mifumo na mbinu mpya za kutibu magonjwa mbalimbali.
Katika ardhi pana ya ulimwengu wa Kiislamu kulijengwa mahospitali mengi yenye zana mpya za kitiba ambazo pia zilikuwa na sehemu na vitengo kadhaa vya kitaalamu. Kwa kadiri kwamba msomi Mfaransa Pierre Rousseau ameandika katika kitabu chake alichokipa jina la "Historia ya Sayansi" kwamba: Mmoja wa wafalme wa Ulaya katika eneo la Bastill nchini Uhispania alipopatwa na maradhi hakuwa na budi isipokuwa kwenda kujitibisha kwa Waislamu wa mji wa Cordoba, makao makuu ya mkoa wa Andalusia.
Kabla ya kuanza mjadala kuhusu mtazamo wa Qur'ani Tukufu juu ya tiba, sina budi kuashiria hapa kwamba japokuwa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kimeashiria kwa njia za moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja kuhusu tiba na utabibu, lakini si kitabu kilichoteremshwa kuzungumzia masuala ya tiba. Qur'ani, kama inavyosema yenyewe, ni kitabu cha kuwaongoza wanadamu katika njia iliyonyooka na kuwadhaminia saada na ufanisi wa dunia na akhera. Ishara za Qurani kuhusu mauala ya tiba na uganga ni thibitisho la elimu isiyokuwa na mpaka ya Mwenyezi Mungu na njia za kumuongoza mwanadamu katika maslahi na hali bora ya maisha. Katibu wa mkutano wa Qur'ani na Tiba uliofanyika Tehran Muhammad Abbasi alisema katika mkutano huo kwamba moja ya miujiza muhimu ya Qur'ani Tukufu ni muujiza wa tiba ambao umewavutia mno wasomi katika pembe mbalimbali za dunia. Amesisitiza kuwa iwapo tutataamali kwa kina katika aya za Qur'ani tukufu, tutaelewa kwamba kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu ni shufaa na tiba ya mwili na roho ya mwanadamu.
Kwa ujumla hapa tunaona bora kuashiria afya ya nafsi na masuala ya kisaikolojia katika Qur'ani Tukufu. Qurani inaitaja imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu kuwa ndio njia bora zaidi ya kutibu maradhi ya kiroho na kinafsi. Inasema katika aya ya 28 ya suratu Raad kwamba:
الَّذِينَ آمَنُواْ وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّهِ أَلاَ بِذِكْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ
"Wale walioamini na zikatulia nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu, kwa yakini, nyoyo hutulia kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu." Katika upande mwingine kitabu hicho kinakutaja kujitenga na kuwa mbali na M, Mungu kuwa ndiyo sababu ya mashaka na matatizo katika maisha ya mwanadamu. Vilevile aya nyingi za kitabu hicho zinawataka Waislamu kuwa na subira na uvumilivu katika kukabiliana na mashaka na masaibu ya aina mbalimbali. Subira hiyo sambamba na kumkumbuka Mwenyezi mungu humpa mwanadamu utulivu wa kiroho. Kwa utaratibu huo uwezo wa kustahamili mashaka wa mwanadamu mwenye imani huongeza na kuwa nguzo imara ya kupambana na masaibu kwa kutumia subira na imani yake kwa Mola Muumba. Uislamu unawafundisha wafuasi wake kwamba ladha na anasa za dunia kwa upande mmoja na mashaka na matatizo kwa upande mwingine ni vitu vya kupita haraka. Hivyo basi mwanadamu anapaswa kujitayarisha kukabiliana na mashaka ya dunia na kuyatambua kuwa ni mtihani wa Mwenyezi Mungu wa kupima kiwango cha imani na uvumilivu wake.
Wakati huo huo katika usia na mafundisho yake, Qur'ani inaashiria baadhi ya masuala ambayo mbali na kuwa na faida za aina mbalimbali hupunguza matatizo ya kiroho na kinafsi. Miongoni mwa masuala hayo ni sisitizo la Uislamu juu na kuoa vijana na kuanza maisha ya ndoa. Sehemu ya aya ya 21 ya suratur Rum inasema: وَمِنْ آیَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَیْهَا
"Na katika ishara zake (Mwenyezi Mungu) amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao.." Uislamu pia unehimiza mno juu ya kuimarishwa uhusiano wa kifamilia na kuunga udugu na jamaa wa karibu hususan mama na baba. Uhusiano huo humfanya mtu awe na uhusiano wa karibu mno na watu wengine na hivyo kubakia salama na mwenye mlingano kinafsi na kisaikolojia. Vilevile Qur'ani inawataka Waislamu kusoma aya za kitabu hicho, kuswali, kuomba dua na amali nyingine za kiibada ili kusafisha roho na kuzidisha amani na utulivu wa moyo. Inawataka kuwa na matumaini kwamba iwapo watamuomba Mola wao kwa dhati, ikhlasi na moyo safi watapata majibu ya maombi yao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Qur'ani kwamba: "Niombeni nitakujibuni."
Katika upande wa afya na tiba ya mwili wa mwanadamu, Qur'ani pia imeashiria nukta kadhaa za kuzingatiwa. Kwa ujumla Uislamu unasisitiza mno juu ya umuhimu wa kujikinga na maradhi mbalimbali. Kwa sababu hiyo aya za Qur'ani na hadithi za Kiislamu zimeashiria baadhi ya amali zinazomkinga mwanadamu na maradhi. Kwa mfano tu, Mtume Muhammad (amani ya M,Mungu iwe juu yake na Ali zake) anausia kwamba: "Msile kabla ya kuhisi njaa, na acheni kula kabla ya kushiba." Vilevile viongozi wa dini wametaja majina ya baadhi ya vyakula ambavyo kuvila au kuacha kuvitumia humkinga mwanadamu na maumivu na maradhi. Qur'ani inasisitiza juu ya taathira ya vyakula kwa roho ya mwanadamu kama inavyosema aya ya 168 ya suratul Baqarah kwamba:
یَا أَیُّهَا النَّاسُ كُلُواْ مِمَّا فِی الأَرْضِ حَلالاً طَیِّبًا وَلاَ تَتَّبِعُواْ خُطُوَاتِ الشَّیْطَانِ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ
"Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri wala msifuate nyayo za shetani, bila shaka yeye kwenu ni adui wa dhahiri."
Kitabu hicho kimeharamisha na kukataza baadhi ya vyakula na vinywaji haramu na visivyokuwa safi na salama ambavyo bila shaka huacha taathira mbaya kwa roho na mwili wa mwanadamu. Miongoni mwa vyakula na vinywaji hivyo ni pombe, nyama ya nguruwe, mizoga na kadhalika. Kitabu hicho vilevile Kinausia kula baadhi ya vyakula ili kwa njia hiyo kudhihirisha hikma na kudura ya Mwenyezi Mungu na kutangaza dawa za kutibu baadhi ya magonjwa. Katika sura ya Qur'ani ambayo Mwenyezi Mungu ameiita kwa jina la "Nyuki" (Nahl) baada ya kueleza utendaji kazi wa mdudu huyo katika ujenzi wa nyumba na kufyonza asali kwenye maua, anasema katika aya ya 69 ya sura hiyo kwamba: "Kinatoka katika matumbo yao kinywaji yaani (asali) cha rangi mbalimbali, ndani yake kina ponyo na shufaa kwa watu.." Mtume Mtukufu (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake anasisitiza pia kwamba hakuna kitu kinachoponya maradhi kama asali. Hii leo pia elimu ya tiba imegundua taathira za asali, suala ambalo limethibitisha mtazamo wa Qur'ani Tukufu.
Maelezo mengine ya kitiba katika Qur'ani ni ufafanuzi unaotolewa na kitabu hicho kuhusu awamu za kuumbika na ukamilifu wa mtoto tumboni mwa mama yake ambao unaoana na elimu ya kisasa. Kitabu hicho kilitangaza tangu karne 14 zilizopita kwamba makazi ya maji ya kiume yanayotunga mimba huwa katika uterasi au mji wa mimba. Qur'ani ilieleza hayo katika kipindi cha giza na ujinga wakati watu walikuwa na fikra zisizokuwa sahihi kuhusu mimba inavyotungika. Kuhusu suala hilo Qur'ani inasema katika aya za 12 hadi 14 za suratul Muuminun kwamba:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الإِنسَانَ مِن سُلالَةٍ مِّن طِينٍ* ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِی قَرَارٍ مَّكِينٍ*ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ فَتَبَارَكَ اللَّهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ.
"Kwa yakini tulimuumba mwanadamu kwa odongo uliosafi. Kisha tukamfanya tone la manii lililowekwa katika makao yaliyohifadhika. Kisha tukalifanya tone hilo kuwa pande la damu, na tukalifanya pande hilo la damu kuwa pande la nyama. Kisha tukalifanya pande hilo la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivisha nyama, kisha tukamfanya kiumbe kingine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji."
Katika sehemu nyingine, Qurani inazungumzia suala la siha na uzima wa mwanadamu. Moja ya mambo yanayozungumiwa na Qur'ani katika uwanja huo ni swaumu na kufunga. Funga ina taathira kubwa na nyingi za kitiba na afya kama anavyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba : "Fungeni mutapata siha." Suala jingine ambalo hatuna budi kuliashiria hapa ni maadili ya kitiba. Suala hilo pia limejadiliwa katika mkutano wa Qur'ani na Tiba. Qur'ani inasisitiza mno juu ya upole, huruma na kuamiliana vizuri baina ya wanadamu. Kwa msingi huo hapana shaka kwamba mwenendo kama huo wa upendo, mahaba na huruma ya daktari kwa mgonjwa unaungwa mkono na kuhimizwa na Qur'ani. Daktari anajihisi kwamba anawajibika kuzingatia roho, nafsi na shakhsia ya mgonjwa wake sambamba na mwili kwa mujibu wa misingi ya kimaadili inayoelezwa na Qur'ani Tukufu. Kwa msingi huo Uislamu unamuusia tabibu na daktari kuwa na mwenendo wa kibinadamu na moyo wa kujituma katika kazi zake. Hivyo basi kutibu wagonjwa hakupasi kuchukua sura ya kimaada na maslahi ya kidunia peke yake. Kwa kuzingatia hayo, washiriki wa mkutano wa Qur'ani na Tiba wametoa wito kwa madaktari kutilia maanani misingi ya akhlaki na maadili na masuala ya kiroho katika muamala wao na wagonjwa.
Tunakamilisha makala hii kwa kunukuu semi ya Dakta Keith Moore, mhadhiri maarufu katika Chuo Kikuu cha Ottawa Canada anayesema: "Kadiri mwanadamu anavyovumbua mambo mapya hugundua kwamba masuala hayo yamekwishatajwa na Qur'ani." Ukweli huo unatokana na hakika kwamba Qur'ani ni kitabu cha Mwenyezi Mungu Muumba wa wanadamu wote, mwenye elimu mutlaki na ni kitabu kamili zaidi kutoka mbinguni.
captcha