IQNA

Qur'ani Tukufu, kimbilio bora katika dunia iliyojaa ufisadi

13:05 - April 19, 2009
Habari ID: 1766827
Kitabu cha Qur'ani Tukufu ndio makimbilio bora zaidi katika dunia ya leo iliyojaa machafuko, ufisadi na matatizo ya kimadaa na kimaanawi yaliyozidishwa na mgogoro wa kiuchumi unaotawala kwa sasa.
Hayo yamesemwa na Ayatullah Nasir Makarim Shirazi, mmoja wa wanazuoni wakubwa nchini Iran. Amesema, katika dunia ya sasa iliyojaa ufisadi na matatizo ya kimaada na kiroho tunapaswa kutafuta makimbilio yatakayotukinga na mawimbi na tufani hizo.
Ayatullah Shirazi amesema hakuna makimbilio bora zaidi ya Qur'ani tukufu, kitabu cha Mwenyezi Mungu (sw) ambacho Mtume Muhammad amesema: Wakati wowote mtakaposhambuliwa na fitina kama usiku wa giza basi shikamaneni na Qur'ani na mtu atakayeifanya Qur'ani kiongozi wake itamuelekeza peponi, na atakayeipa mgongo itamsukuma kuelekea motoni.
Ayatullah Makarim Shirazi amesema kuwa Waislamu hawawezi kukumbwa na tofani kali za kimaada na kiroho iwapo watatekeleza misingi minne ya Qur'ani Tukufu. Kwanza ni kushikamana na kamba imara ya Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani kama inavyosema aya ya 103 ya suratu Aal Imran kwamba: Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu wala msifarikiane. Pili ni kwamba wakati wowote tunapoona mabadiliko katika neema za Mwenyezi Mungu tunapaswa kutambua kwamba sisi pia tumebadilika na hapana budi kufanya marekebisho katika nafsi zetu kwa ajili ya kurejesha neema hizo za Mwenyezi Mungu. Aya ya 11 ya Surat Raad inasema: "Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao."
Tatu ni kwamba iwapo tunataka kufunguliwa milango ya rehma za Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi tunapaswa kuwa na imani na takwa kama inavyosema aya ya 96 ya suratul Aaraf kwamba: "Na lau kama watu wa miji wangaliogopa na kuwa na takwa kwa yakini tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi..". Na nne hatupaswi kuwategemea wageni kwa sababu hilo ni egemeo dhaifu, lisilokuwa na mashiko na hatari. Qur'ani Tukufu inasema: "Wala msiwategemee (mkawa pamoja na) wale wanaodhulumu, usije ukakupateni moto.." (Hud:113)
Tegemeo letu linapaswa kuwa matendo, juhudi na amali zetu wenyewe kama inavyosema aya ya 39 ya suratun Najm kwamba: "Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya."
Ayatullah Makarim Shirazi amesisitiza kuwa ni kwa kuhuisha misingi hiyo minne ambayo ni sehemu ya mafundisho ya Qur'ani Tukufu, ndipo tutakapoweza kushinda matatizo yote ya kimaada ya kiroho. 390153

captcha