Hayo yamesemwa na Hesamudin Farfur Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Fath nchini Syria. Ameongeza kuwa Wamagharibi wanautuhumu Uislamu kwa ajili ya ujahili au kutoujua Uislamu na hilo linatokana na Waislamu kuzembea katika kuuarifisha Uislamu miongoni mwa Wamagharibi.
Msomi hiyo wa Syria amesema: ‘Waislamu hawafanyi juhudi za kutosha kuarfisha ustaarabu wa Kiislamu na ukweli kuhusu maisha ya Kiislamu miongoni mwa Wamagharibi na leo tunalipa gharama za uzembe kuhusu suala hili’.
Ameendelea kusema kuwa Uzayuni umegundua kuwepo wahubiri wachache wa Kiislamu katika ulimwengu wa Magharibi na kwa kutumia uwezo wao wote wanaendesha mikakati ya kuchafua jina la Uislamu na Waislamu. Natija ya jambo hilo ni kuwa Wamagharibi wanaufahamu Uislamu kama watakavyo Wazayuni.
Hesamudin Farfur amesisitiza kuwa Uzayuni unapotosha fikra za Wamagharibi kwa kuunasibisha Uislamu na jinai na ukatili wa Wazayuni.
Kuhusu mazungumzo baina ya Magharibi na Uislamu, msomi huyo wa Syria amesema kabla ya mazungumzo kama hayo Waislamu wanapaswa kufanya mazungumzo baina yao wenyewe na kuimarisha umoja wao.
Mwishoni mwa mahojiano yake, amesema kuwa kujuana, kuhurumiana na kueneza ujumbe wa Uislamu kupitia mazungumzo ni mambo yaliyotiliwa mkazo katika Uislamu. Ameashiria aya zifuatazo za Quran tukufu kuipa nguvu hoja yake. Aya ya 107 ya Suratul Anbiya isemayo: “Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote.” Aya ya 13 ya Suratul Hujurat “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.”
398650