IQNA

Marji'i wa Kidini wapinga filamu potofu kuhusu Imam Hussein (AS) Kuwait

13:10 - May 14, 2009
Habari ID: 1776593
Marji'i na Maulamaa wa kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran wamelalamikia vikali utengenezwaji filamu potofu inayoonyesha nyuso za Imam Hussein (AS) na Imam Hassan (AS) huko Kuwait.
Ayatollah Makarim Shirazi mmoja kati ya Marjaa katika kujibu suali kuhusu filamu hiyo amesema, ‘ filamu hiyo inaenda kinyume cha nyaraka na ukweli wa historia na inalenga kuonyesha kuwa Muawiya na Yazid hawakuwa na kosa’. Amesema filamu hiyo imepuuza nyaraka zote za kihistoria na na ni kinyume na Ijmaa ya wanazuoni wa Kishia. Amesema yamkini lengo la filamu hiyo ni kuibua hitilafu na migogoro baina ya Mashia na Masunni jambo ambalo ni kwa maslahi ya maadui wa Uislamu. Amesema kutayarisha filamu kama hiyo yenye silisili kadhaa ni haramu na kinyume cha maslahi ya Kiislamu na inalaaniwa kwa mitazamo yote.
Aidha Ayatollah Sobhani katika jibu la maandishi kuhusu filamu hiyo amesema watayarishaji wa filamu hiyo hawana nia nzuri katika kufikisha ujumbe na ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu kuchukua hatua za kuzuia utengenezwaji filamu hiyo.
Naye Ayatollah Nuri Hamedani amesema utengenezaji wa filamu hiyo unatokana na ushawishi wa Mawahabi nchini Kuwait. Ametathmini utengenezwaji wa filamu hiyo kuwa katika fremu ya kuendeleza njama sawa na zile za kumvunjia heshima Mtume (SAW) . Mwanazuoni huyo ametoa wito kwa Waislamu wote kuchukua hatua kuzuia kuibuka Salman Rushdie mwingine.
Waziri wa Waqfu wa Syria sehemu ambayo filamu hiyo inatazamiwa kutengenezwa amesema hataruhusu kazi hiyo kuendelea nchini humo bila idhini ya Marjaa wa Kishia. 402762
captcha