IQNA

Mgogoro wa kifedha katika kivuli cha sheria za Kiislamu

12:26 - May 11, 2009
Habari ID: 1776760
Kikao cha kimataifa cha kujadili mgogoro wa kifedha wa kimataifa katika kivuli cha misingi na sheria za Kiislamu, kilifanyika siku ya Jumamosi katika ukumbi wa chuo cha masuala ya kidini na utafiti wa Kiislamu kinachofungamana na Chuo Kikuu cha Sharja nchini Imarati.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Falme za Kiarabu WAM, kikao hicho kilihudhuriwa na idadi kubwa ya wataalamu na watafiti wa masuala ya kiuchumi na sheria za Kiislamu kutoka nchi za Kiislamu na Kiarabu na vilevile za Ulaya. Wazungumzaji katika kikao hicho, mbali na kuchunguza mgogoro wa kifedha unaoendelea hivi sasa duniani pia walijadili misingi na sheria za Kiislamu kwa shabaha ya kutatua mgogoro huo. Mfumo wa kifedha wa Kiislamu kuhusiana na miradi ya uwekezaji na ustawi, ufahamishwaji wa jamii za Kiislamu kuhusiana na thamani na vipimo vya sheria za Kiislamu kuhusiana na masuala ya kiuchumi na kifedha, biashara na benki za Kiislamu ni baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika kikao hicho. Al-Farshi al-Bashir, Mkuu wa Chuo cha Masuala ya Kidini na Utafiti wa Kiislamu cha Sharja amesema katika kikao hicho kwamba, mashirika ya kifedha na benki za Kiislamu hazijaathirika sana na mgogoro wa hivi sasa wa kifedha unaoendelea duniani, jambo ambalo limewapelekea wataalamu wengi wa masuala ya kifedha wa ulimwengu wa Magharibi kusisitiza kwamba njia pekee ya kujikwamua kutoka kwenye mgogoro huo ni kutekeleza mfumo wa kifedha unaozingatia sheria za Kiislamu. 402638
captcha