IQNA

Ayatullah Khamenei asema wanaozusha mifarakano baina ya Shia na Sunni ni vibaraka

13:07 - May 14, 2009
Habari ID: 1778258
Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jumanne Mei 12, 2009 ameonana na mjumuiko mkubwa wa wananchi wa Kurdistan nchini Iran. Kwa mujibu wa Mtandao wa Intaneti wa Kiongozi Muadhamu, mjumuiko huo mkubwa ulijazana katika uwanja wa Uhuru wa mji wa Sanandaj na katika barabara za karibu na uwanja huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru sana wananchi wa mkoa huo kwa mapokezi ya aina ya kipekee waliyompa na kusisitiza juu ya haja ya kulindwa heshima ya taifa. Aidha ametumia fursa hiyo kuzungungumzia kwa upana umuhimu wa kuchagua mtu msafi na anayefaa zaidi katika ujaguzi ujao wa Rais wa Iran kati ya watu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Ayatullah Khamenei ametoa ufafanuzi pia kuhusu sababu za kupatikana heshima na hadhi ya kitaifa nchini Iran likiwa ni suala muhimu mno na la kimsingi na kusema kuwa kulindwa heshima na hadhi ya taifa ni ushahidi wa kuweko maisha sahihi na ya kweli ya jamii iliyojaa fakhari na safi na kwamba ni miongoni mwa sababu kuu zinazolifanya taifa kuwa na istikama na kusimama kidete mbele ya mashinikizo ya maadui wa kigeni. Amesema taifa ambalo katika historia yake na katika utamaduni na uwepo wake halikubali kudhalilishwa na kunyongeshwa ambalo linajivunia kila kilicho chake kama vile mila, desturi, historia na fakhari zake nyingine, taifa hilo huitwa ni taifa linaloheshimu na kulinda hadhi yake. Amesema jambo hilo litawezekana kwa kutegemea mafundisho ya Qur'ani tukufu na kwa kutegemea imani sahihi kwani heshima na utukufu ni maalumu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mtume wa Mwenyezi Mungu na waumini wa kweli wa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei ameashiria pia njama za wakoloni na tawala za vibaraka wao wanaojaribu kupenyeza hisia za kujihisi dhalili ndani ya taifa la Iran na kuongeza kuwa siasa za kujidhalilisha, za kidikteta na chafu za wafalme wa Kiqajari na Kipahlavi nchini Iran mbele ya Uingereza na Marekani zilililetea msiba mkubwa taifa kubwa la Iran katika kipindi cha kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Amekumbusha kuwa, taifa la Iran kwa kutegemea Uislamu na uongozi wa busara wa Imam Khomeini ambaye ni nembo ya heshima ya taifa hili na nchi hii lilisimama kidete kupambana vilivyo na balaa lililosababishwa na tawala hizo za kifalme na ameongeza kuwa, leo hii wananchi wa Iran wanajivunia kwa kuwa kwao Wairani na kwa kuwa kwao Waislamu na kwmba madola ya kibeberu duniani yanakiri kuwa vitisho vyao havina athari yoyote kwa taifa tukufu la Iran na kwa utawala wenye nguvu na wenye ushawishi wa Kiislamu wa taifa hili.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa kulinda heshima ya taifa kunategemea kulinda imani, umoja, nguvu za ushujaa, istikama na kutia nguvu moyo wa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu na kuongeza kuwa, kulinda heshima ya taifa ni nukta ya kimsingi katika michanganuo ya matukio ya kisiasa na kwamba watu wote hususan vijana wanapaswa kuchunguza na kuchanganua kwa kina masuala mbalimbali na kuwa na utambuzi wa kutosha kuhusu sababu za kuendelea kuwepo hadhi ya taifa hili.

Amesema yeyote anayejaribu kuvuruga mshikamano wa taifa ni kibaraka wa adui kwa kujua na kutokujua na kwamba mtu yeyote anayejaribu kuutia dosari mshikamano wa taifa kwa madai ya kutetea imani ya Kisuni au Kishia ni sawa tu mtu huyo awe ni Mshia au Msuni, ajijue kwamba ni mamluki wa adui wa Uislamu na ni sawa tu awe analijua hilo au awe halijui.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria ujinga walio nao baadhi ya vibaraka mamluki wa adui na kuongeza kuwa, makundi ya kisalafi na kiwahabi yanayofanya vitendo vya kigaidi katika nchi za Iraq, Afghanistan na Pakistan hayajijui kuwa ni mamluki wa adui kama alivyo Mshia yoyote yule anayekashifu imani na matukufu ya Waislamu wa Kisuni. Hata kama hatakuwa anajua lakini bado ataendelea kuwa mamluki wa adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa Waislamu wa Kishia na Waislamu wa Kisuni wanaowapenda masharifu na Ahlul Bayt na ambao wanafuata mafundisho ya kiirfani ya Qadiria popote walipo duniani wanahesabiwa na makundi ya Kisalafu na Kiwahabi kuwa ni makafiri, lakini uhakika wa mambo ni kuwa wanaofuata fikra hiyo potofu ni mammluki wa kuleta hitilafu katika safu za Waislamu walio ndugu tangu kale kama ambayo Mshia yoyote yule ambaye anakashifu matukufu ya Waislamu wa Kisuni kwa kukusudia au kutokukusudia alivyo mamluki wa kuleta hitilafu kati ya Waislamu. Kiujumla ni kuwa vitendo hivyo ni haramu kwa makundi yote mawili na ni kinyume cha sheria, amesema.

Aidha amelitaka taifa la Iran kujua thamani ya ushirikiano baina ya serikali na wananchi na serikali nayo ijue thamani ya imani na ushiriki mkubwa wa wananchi na kuongeza kuwa, inabidi kuthamini ubunifu na moyo wa kupenda kazi walio nao wananchi hususan vijana.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema eneo la Kurdisan ni ardhi ya imani, utamaduni na sanaa na ni ardhi ya unyofu, uaminifu na kuongeza kuwa jitihada za wananchi waliopevuka kisiasa wa mkoa huo ambao kwa werevu wao mkubwa waliweza kupambana na njama za adui katika ile miaka ya awali na nyeti kabisa ya umri wa utawala wa Kiislamu nchini Iran kamwe hazitasahaulika ndani ya taifa la Iran.

Amesema wananchi wenye hadhi wa mkoa wa Kurdistan ni watu walioshinda katika mtihani kwani wakati adui alipotumia siasa chafu zilizolenga kuleta mfarakano wa kikabila na kimadhehemu katika jengo adhimu la taifa la Iran, wananchi wa Kurdistan walionyesha kupevuka kwao, wakapambana vilivyo na kuzishinda njama hizo kubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia siasa za utawala wa taghuti wa nchini Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu zilizolenga kuubakisha nyuma kimaendeleo mkoa wa Kurdistan nchini Iran na kuongeza kuwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mkoa huo ulikuwa na wanafunzi 360 tu wa Chuo Kikuu na takriban asilimia 30 tu ya wakazi wa mkoa huo walikuwa wanajua kusoma na kuandika. Amesema wakati huo hakukuwa na miradi yoyote ya maendeleo katika mkoa huo, lakini hivi sasa kuna zaidi ya wanafunzi 40 elfu wa vyuo vikuu mkoani humo wanaopata elimu katika zaidi ya vituo 20 vya elimu ya juu.

Vile vile amesema kazi zilizofanywa na utawala wa Kiislamu katika mkoa wa Kurdistan ni kubwa lakini wakati huo huo amekumbusha kuwa kuna kazi nyingine nyingi zinapaswa kufanywa; kwa hivyo hima zaidi inahitajika kuzifanikisha.

Ayatullah Khamenei amesema suala la kuwepo kaumu na mataifa mbalimbali limo ndani ya Qur'ani na kwamba kwa mtazamo wa viongozi wa Iran, kuweko aina kwa aina ya kaumu na makabila ni fursa kubwa ya kuweza taifa la Iran kujuana zaidi, kuishi kwa usalama na mshikamano kamili na kuweza kutumia vizuri vipaji na uwezo mbalimbali walio nao wananchi.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amezungumzia suala la uchaguzi wa Rais unaotarajiwa kufanyika karibuni hivi nchini Iran na kuongeza kuwa kushiriki kwa wingi wananchi wa matabaka yote katika uchaguzi huo ni suala muhimu sana na kutapelekea kuongezeka heshima na hadhi ya taifa sambamba na kutia nguvu istikama ya nchi na kumkatisha tamaa adui katika tamaa na njama zake za kutaka kuzusha fitna na ufisadi nchini.

Aidha ameashiria juu ya kuguswa na kuumizwa sana adui wa taifa la Iran aliyejaa chuki kuhusu uchaguzi huo na kuongeza kuwa maadui wameanzisha kampeni dhidi ya uchaguzi huo tangu takriban mwaka mzima nyuma na katika propaganda zao wanajaribu sana kukwamisha uchaguzi huo usifanyike kabisa, hilo likiwa ndilo lengo lao kuu lakini ni wazi kwamba hawatafanikiwa kama ambavyo huko nyuma wamekuwa wakifanya njama hizo hizo lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na azma thabiti ya wananchi wa Iran, hila na njama zao zote zimefeli.

Ayatullah Khamenei amesema lengo jengine la maadui katika propaganda zao ni kutaka wananchi wasishiriki kwa wingi katika upigaji kura ili uchaguzi huo ufanyike bila ya hisia zozote lakini amesema wananchi wa Iran watafanya kinyume kabisa na wanavyotaka maadui na kwamba watashiriki kwa wingi na kwa hamasa na utambuzi kamili wa wanachokifanya kwani uchaguzi ni njia ya kuongeza heshima ya taifa na ni miongoni mwa vitu vinavyoonyesha kupevuka kwa taifa.

Amesema Rais wa Iran ana nguvu kubwa na kwamba wananchi wa Iran wanajua na wanashuhudia kwa macho yao kwamba wanapomchagua mtu kuwa Rais wao na akawa ni mtu mchapakazi kikwelikweli, ni kiasi gani ana uwezo wa kuwahudumia na kuwaletea maendeleo wananchi.

Ametoa mwito kwa wananchi wa kumchagua mtu ambaye anayajua na anaumizwa na machungu ya nchi na shinda za wananchi. Amesema suala la kwanza muhimu ni kujitokeza kwa wingi wananchi na suala jengine muhimu katika uchaguzi ujao wa Rais wa Iran ni kuchagua mtu bora na anayefaa zaidi.

Amma kuhusiana na ulazima wa viongozi nchini kujiweka mbali na masuala ya ubadhirifu na matumizi yasiyo ya lazima, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mwaka huu wa 1388 Hijria Shamsia ni mwaka wa harakati ya kuelekea kwenye kurekebisha kigezo cha matumizi na kwamba kupambana na israfu na kulifanya jambo hilo kuwa ndio utamaduni wa taifa kunahitajia miaka mingi ya juhudi zisizochoka. Amesema kama viongozi na jamaa zao watakuwa ni watu wa israfu na kufuja mali, bila ya shaka yoyote hawataweza kuwasaidia kivyovyote vile wananchi katika uwanja huo.

Ayatullah Khamenei amewataka wagombea wa Urais kutumia kampeni zao za uchaguzi kwa njia sahihi na wasitoe matamshi yasiyo na ukweli.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Musa Musawi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala katika eneo la Kurdistan ameashiria hamu kubwa waliyokuwa nayo wananchi wa mkoa huo ya kuonana kwa karibu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema, wananchi wa Kurdistan wametoa maelfu ya mashahidi na majeruhi wa vita katika njia ya kuilinda Iran ya Kiislamu jambo ambalo ni uthibitisho wa wazi wa uhakika kwamba Wakurdi ni sehemu isiyotenganishika na wananchi wengine wa Iran. Aidha amesema, mapokezi makubwa mno aliyopata Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika ziara yake hii ya kuutembelea mkoa wa Kurdistan inathibitisha vizuri jambo hilo. 404240
captcha