IQNA

Kikao cha kimataifa cha Benki za Kiislamu nchini Imarati

14:07 - May 18, 2009
Habari ID: 1779725
Kikao cha kimataifa chini ya anwani 'Benki za Kiislamu, Uhalisia na Matarajio' kinatazamiwa kufanyika tarehe 31 Mei hadi Pili Juni katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati.
Kikao hicho kimeandaliwa na Idara ya Masuala ya Kiislamu na Kheri ya mjini Dubai. Akizungumzia suala hilo, Hamad bin as-Sheikh Ahmad as-Sheibani, mkuu wa kamati inayoshughulikia suala hilo amesema kuwa, wataalamu na wajuzi wa masuala ya kiuchumi wa Kiislamu na wataalamu wa taasisi za kifedha na mifumo ya benki za Kiislamu kutoka nchi mbalimbali za dunia wamealikwa kuhudhuria kikao hicho. Amesema, uwezo wa benki za Kiislamu wa kukidhi mahitaji ya kifedha ya nchi za Kiislamu na athari za mgogoro wa kifedha wa hivi sasa duniani ni baadhi ya mambo yatakayopewa uzito katika kikao hicho. As-Sheibani amesisitiza kuwa kikao hicho kinatazamiwa kuchukua maamuzi muhimu kuhusiana na huduma kwa uchumi wa Kiislamu na njia madhubuti za Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wa hivi sasa wa fedha. Amesema kuwa mfumo wa benki za Kiislamu umesimama juu ya msingi wa sheria za Kiislamu na kuongeza kuwa, hiyo ndiyo sababu ambayo imepelekea kupendwa zaidi benki hizo duniani. Amesema, benki hizo zimekuwa zikifanya vizuri zaidi kifaida na huduma kwa wateja katika baadhi ya sehemu hata kuliko benki za kawaida. 406316
captcha