Kuhusiana na suala hilo, Baraza la Maulamaa wa Kishia nchini Bahrain limetoa taarifa likisema kuwa Ayatullah Bahjat alikuwa nguzo muhimu katika Chuo cha Elimu ya Kidini cha mjini Qum, nembo ya irfan na elimu, mwalimu wa akhlaqi na utakasaji nafsi ambaye alilea na kuwanufaisha wanafunzi wengi kutokana na bahari yake kubwa ya elimu. Baraza hilo limesema kuwa kumpoteza mwanazuoni huyo ni pigo na hasara kubwa kwa vyuo vya kidini na ulimwengu mzima wa Kiislamu. Mashia wa Bahrain siku ya Jumatatu mara tu baada ya kuswali swala za Adhuhuri na Alasiri walikusanyika misikitini na kumuombea fatiha mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu. Magazeti ya kisunni ya nchi hiyo yakiwemo ya al-Wasat na al-Waqt pia yameakisi habari ya kifo cha alim huyo muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu na kutoa salamu za rambirambi kwa Waislamu wote na hasa wa Iran kwa mnasaba huo. 407765