Katika ujumbe wake kufuatia kuaga dunia Ayatullah Bahjat, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alisema, 'Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa marajii wakubwa katika zama hizi, alikuwa ni mwalimu mkubwa wa akhlaki na irfan na alikuwa ni chemchem ya mawimbi ya umaanawi usio na kikomo. Moyo wa mcha Mungu huyo ulikuwa mnyofu na uliojaa nuru, alikuwa ni kioo kilichong'arishwa na ilhamu ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu na alikuwa na maneno ya kuvutia na miongozo ya kifikra na kivitendo kwa wote wanaotafuta njia nyoofu'.
Maisha ya Ayatullah Bahjat
Ayatullah Bahjat alizaliwa maka 1915 katika eneo la Fuman mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baba yake, Karbala'I Muhammad Bahjat alikuwa mtu aliyeaminika na mwenye kutegemewa sana katika eneo hilo.
Ayatullah Bahjat alimaliza masomo yake ya msingi huko Fuman na baadaye kuanza masomo ya kidini hadi mwaka 1929 alipoelekea katika mji mtakatifu wa Qom ili kujiendeleza katika masomo ya lugha ya Kiarabu na fasihi. Baada ya kukaa muda mfupi katika mji wa Qom, Ayatullah Bahjat alielekea katika mji Mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuhudhuria darasa za wanazuoni wakubwa kama vile Ayatullah Sayyid Abul Qasim al-Khu'i.
Mwaka 1933 aliondoka Karbala na kuelekea katika Mji Mtakatifu wa Najaf huko huko Iraq ili kuendeleza masomo ya juu. Akiwa huKo alikuwa kati ya wanafunzi wa Akhund Khurasani. Baada ya kuhudhuria darasa za Ayatullah Dia' al-'Iraqi na Ayatullah Mirza Na'ini', alianza kushirikia katika mihadhara ya Ayatullah Hajj Shaykh Muhammad Husayn al Gharawi al-Isfahani.
Ayatullah Bahjat pia alinufaika sana na mihadhara ya Ayatullahil Udhma Hajj Sayyed Abu Hasan al-Isfahani na Hajj Shaykh Muhammad Kadhim Shirazi.
Mbali na kusoma Fiqhi na Usool, Ayatullah Bahjat vile vile akiwa chini ya usimamizi wa Sayyed Hussein al-Baadkoube'I alisoma kitabu cha 'al-Isharat' cha Ibn Sina na al-Asfari al-Arba'a cha Mullah Sadra Shirazi.
Mwaka 1944, Ayatullah Bahjat alirejea Iran na kuwa mwanafunzi wa Ayatullahil Udhma al Kouhkamar'i's sambamba na kuhudhuria mihadhara ya Ayatullah Boroujerdi katika masomo ya Fiqhi na Usool.
Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Ayatullah Bahjat alikuwa akifunza Fiqhi na Usool katika kiwango cha Kharij nyumbani kwake.
Nasaha za Ayatullah Bahjat
Qur'an
Tumuombe Mwenyezi Mungu asitutenganishe na Qur'an. Sisi kama Waislamu tusitaraji kunufaika na wasio kuwa Waislamu. Tukijetenga na Quran tutakuwa kama wasio kuwa Waislamu.
Umakini katika kumchagua mwalimu
Hakikisha mwalimu wako yuko katika njia nyoofu. Hii ni kwa sababu mwalimu akiwa ameondoka katika mkondo sahihi basi batili yake ataihamishia kwa wanafunzi wake.
Tutende tunayoyajua
Hakuna anayeweza kusema hajui lolote, na akisema atakuwa anadanganya. Tekeleza unayoyajua na usiyoyajua chukua tahadhari katika kuyafanya.
Amali zinazobaki
Wote wajue kuwa wanapaswa kuzingatia amali ambazo zitabaki daima. Amali njema, kumtii Mwenyezi Mungu, Ibada na kile kinachomkurubisha mja kwa Mola ni mambo ambayo hubaki daima.
Mwenyezi Mungu anatuona
Sisi ni wageni wa Mwenyezi Mungu, tuko katika meza yake, anatuona, anajua kila tunalolifanya.
Kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio njia pekee ya saada
Watu wananitaka nitoe mawaidha na nasaha. Iwapo wanakusudia nizungmze na wasikileze basi nawakumbusha kuhusu aya ifuatayo ya Quran Tukufu: " Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." Surat Adh-Dhaariyaat Aya 56.
Uhakika wa Ibada ni kuacha maasia. Wakubwa na wadogo tujue kuwa, njia pekee ya saada na kuokoka katika dunia na akhera ni kumuabudu Mwenyezi Mungu. Ucha Mungu ni kuacha maasia. Kila wakati mja anampomkumbka Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu naye atakuwa naye.
Sala
Fahamu kuwa amali zako zote hutegemea sala yako. Nawausieni kuhifadhi sala tano katika wakati wake.
407845