IQNA

Ayatullah Khamenei:

Ulimwengu wa Kiislamu unahitajia umoja na mshikamano kuliko wakati wowote mwingine

20:57 - July 06, 2009
Habari ID: 1798975
Ayatullah Ali Khamenei leo amehutubia hadhara kubwa ya matabaka mbalimbali ya wananchi kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ameashiria juhudi kubwa za Imam Ali bin Abi Twalib za kusimamisha uadilifu na kulinda umoja na mshikamano katika jamii ya Kiislamu na akasema kuwa haja kubwa zaidi ya ulimwengu wa sasa wa Kiislamu hususan taifa la Iran ni umoja na kuwa macho mbele ya njama za maadui wanaokusudia kuzusha hitilafu miongoni mwao.
Ayatullah Ali Khamenei amewatahadharisha viongozi wa baadhi ya nchi za Magharibi kuhusu jibu la taifa na serikali ya Iran dhidi ya uingiliaji wao katika masuala ya hivi karibuni hapa nchini na akasisitiza kuwa: "Njia ya kushukuru harakati kubwa na mahudhurio ya aina yake ya taifa katika uchaguzi wa Rais wa tarehe 12 Juni na kushiriki karibu watu milioni 40 katika zoezi la kupiga kura, ni kulinda umoja, upendo, kuamiliana vyema, kuchapa kazi na kudumisha harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu miongoni mwa wananchi na wasomi na kutofautisha baina marafiki na maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameashiria nafasi ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu katika kuleta umoja na mshikamano wa taifa la Iran na akasisitiza juu ya udharura wa kulindwa umoja na mshikamano huo. Amesema kuwa uchaguzi wa Rais wa tarehe 12 Juni ambao uliwashirikisha asilimia 85 ya wananchi umeonyesha kwamba Mapinduzi ya Kiislamu nchini yana uwezo wa kukusanya idadi kubwa ya watu katika medani mbalimbali licha ya kupita miaka 30 sasa tangu baada ya ushindi wa mapinduzi hayo, na kwa msingi huo maadui wamejifunga kibwebwe kuzusha hitilafu kati ya wananchi na wamefanikiwa kwa kiwango fulani. Amesisitiza kwamba taifa la Iran linapaswa kuzima njama hiyo.
Ayatullah Khamenei ameashiria siasa za wazi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inatambua ushindani kati ya wagombea wa kiti cha Rais kuwa ni mchuano kati ya watu wa familia moja na akasema: Yumkini ushindani huo wa ndani ya familia ukapeleka kujitokeza hasira baina ya washindani, lakini suala hilo halina mfungamano wowote na wageni.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa lengo la uingiliaji wa maadui katika masuala ya ndani ya Iran ni kuzusha hitilafu na migawanyiko na akaongeza kuwa baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi katika ngazi za Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje, wameingilia waziwazi masuala ya ndani ya taifa la Iran ambayo hayawahusu kisha wakadai kuwa hawaingilii masuala ya ndani ya Iran. "Viongozi hao wamechochea na kuhamasisha machafuko kisha wakawaita wananchi wa Iran kuwa ni watu wanaopenda machafuko na ghasia" amesema Kiongozi Muadhamu.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa watu wanaofanya ghasia na machafuko ni kundi dogo linalotumia bajeti iliyotengwa na baadhi ya nchi za Magharibi kwa ajili ya kazi hiyo na akaongeza kuwa, ni jambo la kawaida kupatwa na huzuni kwa baadhi ya watu ambao mgombea wao ameshindwa, na suala hilo halina maana ya kufanya ghasia na fujo, kwani matokeo ya uchaguzi ni kuwepo waliowengi na wachache. Kwa msingi huo kuwatambulisha wananchi wa Iran katika vyombo vya habari vya Marekani na Ulaya vinavyodhibitiwa na Wazayuni kuwa ni wafanya ghasia na machafuko, ni kulidhalilisha taifa la Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametoa onyo kali kwa viongozi wa baadhi ya nchi za Magharibi na akasisitiza kuwa nchi hizo zinapaswa kuchunga maneno na mwenendo wao wa kiadui kwani taifa la Iran litajibu uadui huo.
Ayatullah Khamenei amesema, Tehran itachukua hatua dhidi ya maneno na mwenendo wa kuingilia mambo ya Iran wa nchi hizo ambao bila shaka utakuwa na taathira mbaya katika mustakbali wa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi hizo.
Amesema kuwa taifa la Iran ni taifa lenye nguvu na mfumo wa Kiislamu hapa nchini umeimarika na kukita mizizi na akasisitiza kuwa hata kama kutakuwepo hitilafu za kimitazamo kati ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini viongozi hao wote huwa na msimamo mmoja katika kukabiliana na adui na kulinda kujitawala kwa taifa. Amesisitiza kuwa maadui wa Iran wanapaswa kuelewa kwamba hawawezi kuzusha mgawanyiko katika ya taifa la Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa viongozi wote wa nchi za kibeberu wanapaswa kuelewa kwamba wananchi wa Iran huwa na neno na msimamo mmoja dhidi ya maadui licha ya baadhi ya hitilafu zao za kimitazamo.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria tajiriba ya miaka thalathini ya uhasama na njama za madola ya kigeni na akazihutubu baadhi ya nchi za Magharibi akisema: "Msidhani kwamba mtaweza kuishawishi baadhi ya mirengo au watu kujiunga nanyi kwa kudai kwamba mnaiunga mkono au kwa kutaja majina ya watu hao; jambo hilo halitatokea abadani, kwani uongo wenu umedhihiri wazi kwa taifa la Iran na linatambua kwamba lengo lenu ni kuzusha hitilafu kati ya wananchi na viongozi wao na kudumisha uhasama dhidi ya serikali ya Kiislamu".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa matumaini na ndoto batili ya baadhi ya nchi za kibeberu ni kuona mfumo wa Kiislamu wa Iran unaojitegemea na unaosimama kidete mbele ya madhalimu hao ukisambaratika na kuongeza kuwa: Madai ya nchi za Magharibi eti ya kuwaunga mkono baadhi ya watu au kuwapinga wengine ni hadaa tupu, kwani kwa mtazamo wa Wamagharibi, kila mtu anayeheshimu mfumo wa Kiislamu, katiba na malengo ya taifa la Iran ni adui wao.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa tajiriba ya miaka thalathini ya kusimama kidete serikali ya Kiislamu na mapigo ya taifa la Iran kwa viongozi madhalimu na wachokozi hadi sasa haijaziamsha baadhi ya nchi za Magharibi na zingali zinakodolea macho kwa tamaa nchi na taifa la Iran. Amesema kuwa kuwa nchi hizo zinakosea na zitaona matokeo ya makosa hayo.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia baadhi ya vibaraka wa vyombo vya propaganda chafu dhidi ya utawala wa Kiislamu wa Iran na akaongeza kuwa, vibaraka hao daima wamekuwepo katika miaka ya huko nyuma. Amesema, watu wa aina hii wanapaswa kuelewa kwamba maadui na mbwa mwitu makatili wanawatumia vibaraka hao kwa ajili ya kukidhi maslahi yao na baadaye watawatupilia mbali kama tambara chafu.
Amesisitiza juu ya udharura wa kuwa macho na kumaizi vyema baina ya rafiki na adui na akasema kuwa, vibaraka hao kadhaa waliohadaika wanatoa ishara za makosa ambazo pia zimewahadaa maadui. Amewataka wananchi, tabaka la wasomi na mirengo yote kuwa macho na kutochanganya baina ya rafiki na adui na hatimaye kuamiliana na rafiki muamala anaostahiki kufanyiwa adui.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kutofautisha baina ya watu wanaovuruga usalama na amani ya wananchi na watu wa kawaida na akasema: Serikali ya Kiislamu itakabiliana na watu wanaovuruga amani na utulivu wa wananchi na kutishia vijana. Hata hivyo ametahadharisha juu ya hatua yoyote ya kumtambua adui kuwa ni rafiki na kumuhesabu rafiki kuwa ni adui kwa sababu ya kosa moja tu.
Ayatullah Ali Khamenei amewataka wananchi kuwa macho na kutomuona adui sugu kuwa ni rafiki na kuhadaika na maneno yake. Amesisitiza kuwa fitina zote zinazofanywa dhidi ya haki na mkabala wa taifa lililomacho zitatoweka na kwa rehema zake Mola, fitina zilizompa matumaini adui katika siku za hivi karibuni zimemalizika.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, haki na kweli ndiyo iliyobakia baada ya fitina na mavumbi yaliyoambatana na fitina hizo na akasema: Hakika na asili ya kubakia ni uchaguzi uliokuwa na msisimko uliohudhuriwa na wananchi karibu milioni arubaini wa Iran walioonyesha tena imani yao kwa serikali ya Kiislamu baada ya kupita miaka 30 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuchaguliwa Rais wa jamhuri kwa kura milioni 24.
Amewahimiza viongozi na wananchi kushukuru na kuthamini neema hiyo kubwa na akasema kuwa wajibu wa viongozi na Rais aliyechaguliwa mkabala wa mahudhurio hayo makubwa ya wananchi ni kuwahudumia wananchi kikamilifu, kutatua matatizo yao, kufanya jitihada za kustawisha nchi na kulinda umoja wa taifa kubwa la Iran.
Amezungumzia pia wadhifa wa wananchi akisema kuwa, taifa la Iran linapaswa kufanya harakati kuelekea upande ulio kinyume na wa maadui ambao ni kulinda umoja, kuwa macho, kupendana, uchapakazi na kudumisha harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu, suala ambalo bila shaka litamridhisha Imamu wa zama Mahdi (as).
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria nafasi aali ya Imam Ali Bin Abi Twalib (as) kwa Mtume Muhammad (saw) na akasema: Maisha ya Amirul Muuminin ni kigezo bora cha malezi ya Kiislamu na yana darsa na ibra nyingi za kufikia saada na ufanisi wa umma wa Kiislamu. Amesema kuwa moja ya darsa za maisha ya Imam Ali (as) ni kupigania haki kwa ajili ya kusimamisha uadilifu na kulinda umoja na mshikamano wa jamii ya Kiislamu ambapo alistahamili mitihani na mashaka mengi katika njia hiyo. Amesema, Imam Ali alifumbia macho haki zake katika baadhi ya mambo kwa ajili ya maslahi ya Uislamu.
Ayatullah Ali Khamenei amekumbusha tena njama za maadui za kutaka kuzusha hitilafu na migawanyiko katika safu za Waislamu na kuwagonganisha Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni na akasema: Kwa sasa ulimwengu wa Kiislamu unahitajia umoja na mshikamano kuliko wakati wowote mwingine na iwapo Waislamu watalinda umoja wao, maadui watashindwa kutumia udhaifu wao kufikia malengo yao.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa mkusanyiko huo mkubwa ulihudhuriwa na wanafunzi wa vyuo vikuu, maimamu wa swala za jamaa, jeshi la kujitolea na familia za mashahidi kutoka mikoa na miji mbalimbali ya Iran. 430342
captcha