IQNA

Ayatullah Khamenei atoa wito kwa Waislamu kutekeleza mafundisho ya Qur'ani

5:59 - July 26, 2009
Habari ID: 1805964
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Jumamosi Julai 25, 2009 ameonana na washiriki wa mashindano ya 26 ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu na kusisitiza kuhusu haja ya Waislamu kujipamba kwa vitendo vyema na kutekeleza ipasavyo mafundisho ya Kitabu hicho Kitakatifu.
Amesema kutekeleza ipasavyo mafundisho ya Qur'ani kutaufanya Ummah wa Kiislamu upate heshima, maendeleo, adhama na mshikamano. Amegusia pia umuhimu wa kulindwa umoja na mshikamano nchini Iran na kuongeza kuwa, matukio yaliyotokea hivi karibuni nchini yasiwe sababu ya kuzusha hitilafu na mifarakano na kwamba kila mmoja anapaswa kushirikiana na wenzake kiudugu kwa ajili ya kuliletea maendeleo taifa.

Mkutano huo umefunguliwa kwa Qur'ani Tukufu iliyosomwa na Mabwana Abul Qasemi, Mhadhiri na Jaji wa Kimataifa wa mashindano ya Qur'ani, Husaini, mshindi wa kwanza wa usomaji tajwidi, Zavidat, mshindi wa kwanza wa kuhifadhi Qur'ani nzima na Ustadh Abdul Fatah Taruti, jaji wa kimataifa wa Mashindano ya Ishirini na Sita ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyomalizika Ijumaa Julai 24, 2009 mjini Tehran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema lengo la kufanyika mashindano kama hayo ya Qur'ani Tukufu ni kuzidi kuwa na mfungamano na Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Vile vile ameashiria kwamba haitoshi kustafidi na Qur'ani kwa macho na masikio tu bali nyoyo zetu nazo zinapaswa kufaidishwa na Qur'ani. Amesisitiza kuwa, Qur'ani ni Kitabu kwa ajili ya kufanyiwa kazi yaliyomo ndani yake, kukielewa ipasavyo na kutafakari miongozo yake na kwamba athari na faida za Qur'ani zinapatikana kwa kiwango kile kile tutakayofanyia kazi mafundisho yake.

Amesema kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwanusuru waumini lazima itatimia na kuongeza kuwa kwamba iwapo tutatimiza masharti ya kupata nusra ya Mwenyezi Mungu na kutekeleza maamrisho ya Qur'ani Tukufu basi bila ya shaka tutaweza kupata nusura hiyo ya Mwenyezi Mungu katika maisha yetu.

"Leo hii ulimwengu wa Kiislamu una kiu ya kutekeleza mafundisho ya Qur'ani na inabidi Qur'ani iwe kigezo, marejeo na mhimili wa maarifa na matendo yetu." Amesema.

Aidha katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia njama za maadui wa Uislamu na Qur'ani Tukufu za kutaka kuharibu mshikamano wa Kiislamu na kuzitia roho mbaya nyoyo za uma wa Kiislamu ili Waislamu waonane maadui na wachukiane na kusisitiza kuwa, maadui wanatumia hila na hadaa kutaka kuwafumba macho watu.

"Wanadai wao hawapingi Qur'ani lakini wanachopinga ni malezi na mafunzo yaliyomo ndani ya Qur'ani" Amesema.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia umoja na mshikamano wa taifa la Iran na kuongeza kuwa, maana ya kuwa wamoja na wenye kushikamana katika kamba ya Mwenyezi Mungu ni kwa wote kuwa kitu kimoja ijapokuwa wanaweza kuwa na tofauti katika baadhi ya mambo madogo madogo na kwamba hilo halizuii kupatikana mshikamano na umoja.

Vile vile ametoa mwito wa kuchunga maneno na matendo yasije yakazusha ugomvi na hitilafu na kuongeza kuwa, kuwafukuza na kuwakataa wengine kwa sababu ya mambo ya daraja la pili si jambo sahihi na kila mmoja anapaswa kushirikiana kidugu na wenzake kwa ajili ya kujenga nchi na kuiletea maendeleo.

Ameashiria pia mambo ya siku mbili tatu zilizopita yaliyojiri nchini Iran na kusema jambo hilo dogo halipaswi kukuzwa na kuleta mifarakano. Pia amesema si sahihi kumtuhumu mtu na kumuona hafai kwa sababu ya suala moja au mawili wakati kuna masuala mengine mengi mazuri aliyoyafanya.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amemtaka kila mtu awe na insafu na uadilifu katika matendo na maneno yake. Ameashiria pia mafundisho na usia uliomo katika Qur'ani tukufu wa kuwataka watu wawe na insafu na uadilifu hata katika kuamiliana na maadui na kuongeza kuwa, inabidi katika utawala wa Jamhuri ya Kiislamu watu wote wawe wamoja sambamba na kulinda misingi na mitazamo yao.

Amesema kutofautiana kimawazo ni jambo la kawaida na la kimaumbile. Amegusia pia kuwa katika serikali zote zilizopita kumeshuhudiwa tofauti za mitazamo na kuongeza kuwa, mambo huharibika wakati tofauti hizo za mitazamo zinapochanganyika na hawaa na matamanio ya nafsi hivyo inabidi watu waangalie misimamo yao na kuona ipi imechanganyika na matamanio ya nafsi na ipi wanaichukua kiikhlasi na kutekeleza wajibu wake mtu.

Amesema wakati mtu anapokuwa makini katika kutekeleza jukumu lake na kuchunga taqwa katika matendo yake mtu huyo hupata radhi za Mwenyezi Mungu.

Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharua wa kufanya juhudi kwa ajili ya kutekeleza vilivyo majukumu na wakati huo huo kuwa na taqwa katika matendo. Ameoingeza kuwa, Alhamdulillah hadi sasa Mwenyezi Mungu amekuwa akilisaidia na kulitia baraka taifa la Iran.

Katika mkutano huo Hujjatul Islam Walmusilimin Muslihi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi za Qur'ani zinazofanyika nchini na kuongeza kuwa taasisi yake imeweza kukifanya Kitengo cha Mafunzo ya Qur'ani Vyuoni kuwa Chuo Kikuu cha Elimu na Maarifa ya Qur'ani nchini.

Vile vile amesema katika Mashindano ya mwaka huu ya Ishirini na Sita ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu, wawakilishi 94 kutoka nchi 55 duniani wameshiriki katika mashindano hayo na kwamba baadhi ya ratiba zilizokuwemo kwenye mashindano hayo ni kwa mara ya kwanza kushuhudiwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
438716

captcha