IQNA

Nchi 59 zakubali kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Misri

9:57 - August 11, 2010
Habari ID: 1970917
Abdul Qadir Sarhan, msimamizi mkuu wa mashindano ya 18 ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu nchini Misri amesema kwamba nchi 59 zimekubali kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani yatakayoandaliwa hivi karibuni nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti la nchi hiyo la al-Masr al-Yaum, akitangaza habari hiyo mbele ya waandishi habari katika Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu Abdul Qadir Sarhan amesema kuwa mashindano hayo yatafanyika katika ukumbi wa Imam Muhammad Abduh wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar kuanzia tarehe 18 ya mwezi wa Ramadhani na kuendela hadi tarehe 27 mwezi huohuo. Ameendelea kusema kuwa Wizara ya Wakfu ya Misri tayari imewachagua marefa 9 wa Qur'ani kutoka nchi za Syria, Lebanon, Tunisia, Imarati, Senegal, Saudi Arabia, Sudan, Libya na Morocco na wanne kutoka Misri kwa shabaha ya kusimamia mashindano hayo.
Bwana Sarhan ameendelea kusema kuwa mashindano hayo yatafanyika katika marhala tano ambazo ni kuhifadhi Qur'ani nzima kwa kutumia mbinu ya tartil na tajweed pamoja na tafsiri ya juzuu ya 16 ya Qur'ani, kuhifadhi Qur'ani nzima, kuhifadhi juzuu 20 za Qur'ani, kuhifadhi juzuu 10 na hatimaye kuhifadhi juzuu 6 za kitabu hicho kitakatifu, maalumu kwa wasiokuwa Waarabu. 630128
captcha