IQNA

Maonyesho ya turathi za kielimu za ulimwengu wa Kiislamu kufanyika Uturuki

15:49 - August 12, 2010
Habari ID: 1972025
Uturuki imepanga kuandaa maonyeso ya kimataifa ya turathi za kielimu za ulimwengu wa Kiislamu ambazo zimeathiri zaidi ustaarabu wa mwanadamu katika kipindi chote cha historia.
Moanyesho hayo yataanza tarehe 17 mwezi huu wa Agosti. Kwa mujibu wa tovuti ya World Bulletin, maonyesho hayo yana lengo la kuonyesha juhudi kubwa zilizofanywa katika ulimwengu wa Kiislamu na hasa katika kipindi kinachotajwa kuwa ni kipindi cha kunawiri Uislamu, yaani kipindi cha kati ya karne ya 8 hadi 13 Milaadia, katika kustawisha utamduni wa mwanadamu. Kipindi cha kunawiri Uislamu au kwa ibara mashuhuri zaidi 'Kipindi cha Dhahabu katika Uislamu' ni kipindi ambacho ulimwengu wa Kiislamu ulishuhudia maendeleo na ustawi mkubwa wa kielimu, kiutamaduni, kisanaa na kiteknolojia, maendeleo ambayo yalikuwa msingi wa maendeleo na ustawi wa ustaarabu wa nchi za Ulaya.
Akiwa safarini mjini London Uingereza mwezi Machi uliopita, Rajab Tayyib Erdogan Waziri Mkuu wa Uturuki aliomba maonyesho hayo yaliyokuwa yakifanyika mjini humo yafanyike nchini kwake pia. Kwa msingi huo, wakaazi wa Istanmbul ambako ndiko maonyesho hayo yatafanyika wanaweza kuwa na matumaini ya kushiriki bila malipo katika maonyesho hayo ambayo yaliwavutia watu laki nne mjini London.
Akizungumzia suala hilo, Salim al-Husna, Mkuu wa Taasisi ya Sayansi, Teknolojia na Ustaarabu ya Uturuki FSTC ambaye pia ni msimamizi wa maonyesho hayo amesema kuwa nafasi muhimu ya kielimu na kiutamaduni ya China, India na nchi za Kiislamu katika kipindi kilichotajwa barani Ulaya kuwa 'kipindi cha giza,' itazingatiwa katika maonyesho hayo. 631402
captcha