Katika hotuba za Sala ya Ijumaa y mjini Tehran, Ayatullah Ahmad Jannati amesema kuwa kila mara taifa la Iran linapohisi Marekani inasisitiza juu ya jambo fulani, kwa uangalifu hugundua chanzo cha sisitizo hilo kwani wananchi wanajua kwamba Marekani ni adui wao mkubwa. Akihutubia halaiki kubwa ya waumini katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran, Ayatullah Jannati amesema kadhia ya vikwazo ni moja ya jinai za Marekani dhidi ya taifa la Iran. Ameongeza kuwa Marekani inalizulia taifa la Iran matatizo na kutumia vikwazo ili lisalimu amri lakini haijui uwezo wa taifa kubwa la Iran.
Ayatullah Jannati ameashiria jinai mbalimbali za Marekani dhidi ya taifa la Iran na kusema kuna nyaraka za kutosha na zisizopingika kuhusi jinai hizo.
Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Jannati ameashiria siku ya leo Jumamosi Agosti 14 ambayo ni siku ya kumbukumbu ya ushindi wa harakati ya mapambano ya Lebanon dhidi ya Wazayuni na kusema: "Wanamapambano shupavu na wenye imani wa Hizbullah walipambana na Wazayuni kwa kipindi cha siku 33 na hatimaye kuulazimisha utawala wa Kizayuni kusalimu amri kwa madhila". Amesisitiza kuwa, Marekani na Utawala wa Kizayuni bado zingali zinafedheheka kutokana na ushindi huo ambao ulikuwa pigo kubwa kwa tawala hizo mbili.
632250