IQNA

Pakistan kuandaa vikao kadhaa vya kuwaunga mkono Wapalestina

12:13 - August 18, 2010
Habari ID: 1976135
Taasisi ya Kuwaunga Mkono Wapalestina ya nchini Pakistan PLF imetangaza kwamba imepanga kuandaa vikao kadhaa vya kimataifa katika miji muhimu ya nchi hiyo katika mwezi huu wa Ramadhani.
Kwa mujibu wa tovuti ya Shianews, Swabir Karbalai, msemaji wa taasisi hiyo amesema kuwa vikao hivyo vitafanyika katika miji ya Islamabad, Karachi, Lahore, Kuweita na Pishawar kwa ajili ya kutangaza mfungamano na mshikamano na watu wa Palestina, hasa katika kipindi hiki kigumu cha kukandamizwa na kuzingirwa na utawala haramu wa Israel.
Ameendelea kusema kuwa mkanda wa hotuba zilizotolewa hivi karibuni na viongozi wa makundi ya Kiislamu na mapambano ya Palestina utaonyeshwa katika vikao hivyo. Viongozi wa kidini na kisiasa wa Pakistan wamepangiwa kuzungumza katika vikao hivyo.
Huku akisisitiza kwamba uungaji mkono kwa watu wa Palestina ni jukumu la kidini, kijamii na kimaadili kwa Waislamu, Karbalai amesema kuwa vikao hivyo vinafanyika kutokana na ombi lililotolewa hivi karibuni na mkuu wa Taasisi ya Kuwaunga Mono Wananchi wa Palestina ya nchini Pakistan, kwa vyama na makundi ya kisiasa na kidini katika mwezi huu wa Ramadhani, kwa madhumuni ya kuwaunga mkono Wapalestina na kukabiliana na hatua za ukandamizaji za utawala ghasibu wa Israel dhidi yao. 635792
captcha