Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) ametoa taarifa akizitaka nchi za Kiislamu zichukue hatua za haraka kwa lengo la kuwafikishia misaada ya dharura wahanga wa mafuriko nchini Pakistan.
Huku akiashiria kiwango kidongo cha misaada ya kimataifa ambayo hadi sasa imepelekwa nchini Pakistan, Ihsanoglu amesema kuwa wananchi Waislamu wa nchi hiyo wanakabiliwa na matatizo mawili makuu ambayo ni vita vya kikabila katika maeneo tofauti kwa upande mmoja na mafuriko kwa upande wa pili. Amesema kwa kuzingatia hali hiyo, Waislamu wanapasa kutekeleza vyema jukumu lao la kiutu la kuwasaidia Waislamu wenzao wa Pakistan ambao wameathirika na mafuriko hayo kwa lengo la kumridhisha Mwenyezi Mungu hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhani. Amebainisha matumaini yake kwamba wanachama wa kudumu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu watafanya kikao cha dharura kwa ajili ya kujadili mkasa wa mafuriko wa Pakistan na kutafuta njia zinazofaa kwa lengo la kutuma nchini humo misaada ya kibinadamu haraka iwezekanavyo. Ameashiria ukubwa na upana wa mafuriko hayo pamoja na matatizo yanayotatiza shughuli za ufikishaji misaada kwa waathirika na kuelezea matumaini yake kwamba katika kikao chao cha dharura, nchi 57 wanachama wa OIC zitachunguza njia zinazofaa kwa ajili ya kufikisha misaada ya dharura kwa watu waliopoteza makazi yao kutokana na mafuriko hayo.
Ihsanoglu pia amezitaka jumuiya za hilali nyekundu za nchi za Kiislamu kufanya vikao vya dharura kwa ajili ya kuchunguza njia za kuwashughulikia wahanga wa janga la mafuriko nchini Pakistan. Pia amezitaka nchi za Kiislamu kupata funzo kutokana na janga hilo na kujiandaa vilivyo kwa lengo la kukabiliana na majanga mengine ya kimaumbile. 636347