Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo huadhimishwa kote ulimwenguni katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, itaadhimishwa nchini Tanzania katika msikiti wa Kichangani ulioko katika mji mkuu, Dar es Salaam.
Akizungumzia jambo hilo katika mahojiano maalumu na shirika la habari za Qur'ani IQNA, Mustafa Ranjabar, muambata wa utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania amesema katika siku za hivi karibuni maimamu wa swala za jamaa wa misikiti ya Shia na Suni wakishirikiana na jumuiya za Kiislamu wamekuwa wakikutana na kufanya vikao vya kutayarisha ratiba na mipango itakayotekelezwa katika siku hiyo.
Amesema Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania ambacho kimekuwa katika mstari wa mbele wa kuandaa maadhimisho hayo, kimekuwa kikishirikiana na wawakilishi wa mashirika na makundi mbalimbali yaliyo na hamu ya kushiriki katika shughuli hiyo muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu ili kuyafanikisha maadhimisho hayo.
Ranjbar ameendelea kusema kuwa hutuba za mabalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Palestina na Syria wanaohudumu nchini Tanzania kuhusiana na umuhimu wa Quds Tukufu kwa Waislamu wote, maonyesho ya vitabu na picha zinazohusiana na Quds Tukufu na kusambazwa bidhaa za kiutamaduni zikiwemo CD zinazohusiana na Palestina ni miongoni mwa mambo yatakayotekelezwa katika siku hiyo. 644169