IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Dubai kumalizika leo

18:12 - August 30, 2010
Habari ID: 1984596
Sherehe za kuhitimisha Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani zawadi ya Dubai na kuwaenzi washindi wa mashindano hayo zinafanyika hii leo Jumatatu.
Shakhsia wa Kiislamu katika mwaka huu wa 2010 pia wataenziwa katika sherehe za kuhitimisha mashindano hayo.
Washindani 70 katika kuhifadhi Qur'ani nzima kutoka nchi mbalimbali walichuana katika kipindi cha siku kumi. Washindani wengine 8 hawakuweza kuingia fainali baada ya kushindwa katika awamu ya kwanza ya mashindano hayo.
Jumamosi ya juzi tarehe 28 Agosti Sayyid Muhammad Rizqi kutoka Indonesia, Sayyid Muhammad Mahamadou wa Mauritania, Nasir Badr Muhammad kutoka Kuwait na Mbwana Issa kutoka Tanzania walichuana katika kuhifadhi Qur'ani nzima kwa mujibu wa riwaya ya Hafs.
Kamati iliyosimamia Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Dubai pia imemchagua rais wa zamani wa Sudan Abdul Rahman Swar al Dhahab kuwa Shakhsia wa Kiislamu wa mwaka huu wa 2010. Swar al Dhahab kwa sasa anasimamia Jumuiya ya Kimataifa ya Ulinganiaji wa Kiislamu na ametoa huduma kubwa kwa Uislamu na Waislamu katika nchi mbalimbali duniani.
Baadhi ya huduma kubwa za shakhsia huyo wa Kiislamu ni pamoja na kufanya jitihada za kujenga zaidi ya misikiti 2000 katika nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya mashariki, kushiriki katika ujenzi wa vituo 6 vya kulea mayatima katika nchi za Kiafrika na jitihada za kuasisi vituo vya Kiislamu, shule, zahanati na mahospitali kwa ajili ya Waislamu kwenye nchi maskini za Kiafrika.
Mashindano ya 14 Kimataifa ya Qur'ani Tukufu zawadi ya Dubai yalianza Jumatano iliyopita katika Chumba cha Biashara na Viwanda cha Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu. 644629

captcha