IQNA

Jumuiya ya Nchi za Kiislamu yalaani mchezo unaohujumu Uislamu

12:59 - September 05, 2010
Habari ID: 1987818
Msemaji wa kitengo cha kukabiliana na hujuma zinazoulenga Uislamu cha Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ametoa taarifa akilaani mchezo wa intaneti uliotayarishwa na chama cha Uhuru cha Austria unaohujumu Uislamu.
Msemaji huyo wa OIC amesema, katika mchezo huo uliopewa jina la 'Kwaheri Msikiti', mchezaji anapaswa kulenga misikiti, minara na waadhini wa misikiti. Amesema michezo kama hiyo ni kielelezo cha propaganda za kuwafanya watu wauogope Uislamu barani Ulaya na umewachukiza mno Waislamu wa Austria na maeneo mengine duniani.
Amesema inasikitisha kuona katika nchi kama Austria ambako Uislamu unatambuliwa kuwa ni miongoni mwa dini rasmi kunajitokezsa chama cha siasa kinachodhalilisha matukufu ya Kiislamu kwa shabaha ya kupata kura zaidi katika uchaguzi, suala ambalo limewakasirisha mno Waislamu kote duniani.
Msemaji wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ameongeza kuwa kutolewa mchezo huo kumeleta changamoto nyingi kwani unakabiliana na juhudi za kimataifa za kueneza moyo wa maelewano na uvumlivu kati ya dini mbalimbali.
Ameishukuru serikali ya Austria kwa kupiga marufu mchezo huo na akaelezea matumaini ya kutoshuhudiwa tena vitendo vya kudhalilisha matukufu ya dini na kuchochea hisia za wafuasi wa dini nchini humo.
Viongozi wa Austria wamepiga marufuku mchezo wa Kwaheri Msikiti uliotayarishwa na chama chenye misimamo mikali cha mrengo wa kulia ambao umekosolewa vikali na vyama vingine vya siasa, jumuiya za Kiislamu na kanisa Katoliki la Austria. 648365

captcha