IQNA

ISESCO yataka adhabu kali ichukuliwe dhidi ya wanaobeza dini

11:47 - September 12, 2010
Habari ID: 1991713
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Nchi za Kiislamu ISESCO, limeutaka Umoja wa Mataifa kubuni sheria ya kimataifa ya kukabiliana na watu wanaokebehi na kubeza matukufu ya dini. Ikitoa radiamali kuhusiana na wito uliokuwa umetolewa hivi karibuni na Kasisi Terry Jones wa jimbo la Florida nchini Marekani la kutaka kuchomwa moto Qur'ani Tukufu, ISESCO imeutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za lazima haraka iwezekanavyo kuhusiana na suala hilo.
Kupitia taarifa, ISESCO imesema kuwa kukaririwa kwa vitendo vya ubezaji dhidi ya matukufu ya dini kunathibitisha wazi kwamba hakuna sheria ya kimataifa iliyobuniwa kuwazuia watu waovu kuendelea kufanya vitendo kama hivyo vya dharau dhidi ya matukufu ya kidini, jambo linalokwenda kunyume kabisa na misingi ya thamani za maadili ya kiutu.
Katika taarifa hiyo ISESCO imewataka Waislamu kuendelea kuzingatia maadili matukufu ya Uislamu katika kukabiliana na vitendo hivyo vya kichochezi dhidi ya Uislamu na kufanya juhudi maradufu za kueneza mafundisho ya dini hii katika pembe zote za dunia. Imewataka kurekebisha sura potofu inayoenezwa na waovu kuhusu Uislamu duniani na kusema hilo ndilo litakalokuwa jibu madhubuti zaidi kwa hujuma inayoenezwa na wabaguzi na watu walio na chuki dhidi ya Uislamu.
Terry Jones aliye na kanisa dogo lenye wafuasi 50 tu katika Jimbo la Florida alitaka kuchoma Qur'ani kwa mnasaba wa mashambulio ya Septemba 11 nchini Marekani jambo alilolazimika kulipuuzilia mbali baada ya kukabiliwa na wimbi kali la ukosoaji kutoka kwa Waislamu na Wakristo ulimwenguni. 652518
captcha