Kwa mujibu wa gazeti la Misri la Alyaum as-Sabe' Ahmad Atayyib, Sheikh wa al-Azhar amesikitishwa mno na hatua ya kundi hilo alilolitaja kuwa la watu wachache nchini Marekani, ya kuchana na kisha kuchoma kurasa za kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Huku akitaja kitendo hicho kuwa duni na dhaifu mno ambacho hakiwezi kudhuru kwa njia yoyote ile Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Sheikh wa al-Azhar amesema kuwa kundi hilo lenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu sio wawakilishi wa mataifa ya Magharibi kwa sababu wanafikra na wasomi wengi wa mataifa hayo wamelaani na kukosoa kitendo hicho.
Ahmad Tayyib amesisitiza katika taarifa hiyo kwamba Waislamu wanaheshimu dini zote na kwamba wanaamini kuwepo uhusiano mzuri miongoni mwa wafuasi wa dini hizo licha ya kuwepo tofauti za kiitikadi baina yao. Hata hivyo amasisitiza kwamba umma wa Kiislamu kamwe hautavumilia kubezwa na kudharauliwa matukufu yake ya kidini.
Tunakumbusha hapa kuwa licha ya Terry Jones kutupilia mbali uamuzi wake wa kutaka kuchoma Qur'ani tarehe 11 Septemba huko Florida, lakinii baadhi ya Wakristo wenye misimamo ya kupindukia mipaka walichukua uamuzi wa kuchoma moto kitabu hicho kitakatifu mbele ya White House mjini Washington katika siku ya Jumamosi ambayo ilisadifiana na tarehe 11 Septemba siku ya kumbukumbu ya matukio ya kigaidi nchini Marekani. Vilevile makasisi wawili wasiojulikana sana katika jimbo la Tennessee walichukua hatua ya kuchoma tarjumi mbili za Qur'ani mbele ya kundi ndogo la watu wakiwemo waandishi habari wa kieneo. 653376