Kwa mujibu wa tovuti ya kituo hicho, kituo hicho kimesema kuwa wito wa Kasisi Terry Jones wa Kanisa la Dove World Outreach la jimbo la Florida nchini Marekani, wa kutaka kuchomwa kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika maadhimisho ya mwaka wa tisa wa matukio ya kigaidi nchini Marekani, ni hatua ya kiuadui na kiburi unayokwenda kinyume kabisa na misingi ya kiakili na kidini ya dini zote za mbinguni. Imesema kuwa ukweli huo unatokana na kuwa dini hizo zote zinatoa wito wa kuheshimiwa mafundisho ya dini zote za mbinguni na kwamba Qur'ani inawataka Waislamu wote kutotofautisha wala kuwabagua mitume wa Mwenyezi Mungu. Tarifa hiyo imesema kuwa wito wa kasisi huyo unadhihirisha maradhi yake ya kinafsi na kiakili kwa sababu amedharau na kukejeli kitabu kitakatifu kinachofuatwa na zaidi ya Waislamu bilioni moja duniani na kwamba jambo hilo haliwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote na madai ya uhuru wa kusema na kujieleza, kwa sababu uhuru kama huo hauruhusu kukanyagwa matukufu na haki za watu wengine. Taarifa hiyo imesisitiza kwamba dini zote zinapasa kukemea na kulaani hatua kama hizo za dharau dhidi ya matukufu la sivyo mlango wa kushambuliwa na kubezwa matukufu ya kidini utakuwa umefunguliwa kwa waovu wanaotaka kueneza dharau dhidi ya matukufu hayo duniani. 655938