IQNA

Ihsanoglu ataka kulaaniwa vitendo vya ubaguzi wa rangi

12:33 - September 18, 2010
Habari ID: 1995900
Ekmeleddin Ihsanoglu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ametaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wabaguzi wa rangi na pia watu wanaowabagua wafuasi wa dini mbalimbali.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP Ihsanoglu aliyekuwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko mjini Geneva Uswisi amesisitiza kwamba marufuku ya kujengwa minara na misikiti, wito wa kuchomwa moto Qur'ani Tukufu na kubuniwa makundi yanayounga mkono vitendo vya ghasia na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu ni baadhi ya mambo yanayopaswa kupingwa na kufuatiliwa kisheria katika duru za kimataifa.
Amesema vitendo kama hivyo miongoni mwa raia wa taifa moja huleta unafiki, misimamo ya kupindukia mipaka na hitilafu katika taifa hilo.
Ihsanoglu amemtaka Kamishna Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu kumteua mwakilishi wake ambaye atakuwa na jukumu la kukusanya habari kuhusiana na vitendo vya ubaguzi wa rangi, ubaguzi dhidi ya wafuasi wa dini tofauti na makundi yanayounga mkono vitendo vya ghasia kote ulimwenguni. Mwishoni mwa hutuba yake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ameutaka Umoja wa Mataifa kutumia uwezo wake wote kwa ajili ya kupambana na dharau dhidi ya matukufu ya kidini. 656521
captcha