IQNA

Kikoa cha kimataifa cha Uislamu na Mazungumzo ya Tamaduni chafanyika nchini Hispania

13:59 - September 25, 2010
Habari ID: 2000772
Kikao cha kimataifa cha Uislamu na Mazungumzo ya Tamaduni kimefanyika katika mji wa Saraqusta au kwa jina jingine Zaragoza nchini Hispania tokea siku ya Alkhamisi.
Kikao hicho kimeandaliwa na Chuo Kikuu cha Saraqusta. Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Kuwait KUNA, wataalamu, watafiti na wasomi katika nyanja za utamaduni wa Kiislamu na mbinu za kuishi pamoja kwa amani Waislamu na Wakristo, kutoka pembe mbalimbali za dunia likiwemo bara Ulaya wameshiriki katika kikao hicho. Washiriki wamejadili mambo mbalimbali yakiwemo ya kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa tamaduni na staarabu tofauti na uhusiano wa kiutamaduni kati ya Uislamu na ulimwengu wa Magharibi.
Changamoto zinazowakumba Waislamu katika nchi za Magharibi, mbinu za kuishi pamoja kwa amani pande mbili katika kivuli cha kuvumiliana kiutamaduni na kiustaarabu katika mazingira ya kiidara, ni mambo mengine ambayo yamepewa uzito katika kikao hicho cha siku mbili. Akizungumza katika kikao hicho meya wa mji wa Zaragoza amesema kuwa kufanyika kwa kikao hicho mjini humo kunathibitisha wazi mazingira mazuri ya kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa tamaduni mbalimbali katika mji huo.
Amebainisha pia mipango ya kujengwa kituo cha utamaduni wa Kiislamu katika mji huo katika siku zijazo na kuongeza kuwa Waislamu wapatao 20,000 wanaoishi katika mji huo watapata fursa ya kutekeleza shughuli zao za kiutamaduni kwa uhuru kamili katika kituo hicho bila kubughudhiwa na mtu yoyote. 661584
captcha