Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, viongozi wawili hao waliokuwa wakizungumza hivi karibuni katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York wamesisitiza juu ya kuimarishwa utamaduni wa kuvumiliana kidini ulimwenguni.
Akizungumzia suala hilo, Ahmad Abdul Ghait, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa inasikitisha kuona kwamba Waislamu katika baadhi ya nchi za Magharibi wanasumbuliwa, kukejeliwa na kutusiwa matukufu yao ya kidini kutokana na imani zao. Amesema, Misri itafanya kila liwezekanalo katika nyanja za kisiasa na kiutamaduni ili kukabiliana na tishio hilo ambalo amesema linatokana na ujahili wa baadhi ya watu.
Amezitaka nchi za ulimwengu kutekeleza vilivyo majukumu yao ya kukabiliana na vitendo hivyo vilivyo dhidi ya dini na kuimarisha utamaduni wa kuvumiliana, kupambana na fikra finyu, chuki na kubuni sheria za kulinda makundi na jamii za wachache.
Kwa upande wake Moulaye Ould Mohamed Laghdaf, Waziri Mkuu wa Mauritania amekosoa kuhusishwa Uislamu na vitendo vya ugaidi na kuongeza kuwa jambo hilo limekuwa na athari mbaya sana kwa nchi yake. Amesisitiza kuwa serikali ya nchi yake imefanya juhudi kubwa za kupambana na ugaidi na pia kuimarisha nafasi ya maulama katika kuwasilisha fikra sahihi ya mafundisho ya Kiislamu ambayo yanahimiza upendo, takuwa, kusameheana na amani duniani. 663383