Huku akilaani hatua hiyo, Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa OIC amesema katika taarifa hiyo kwamba kuchapishwa kwa vikatuni hivyo vinavyokejeli matukufu ya Kiislamu katika mfumo wa kitabu ni sawa na kudharau hisia za Waislamu wote duniani.
Amesema jukumu la kimaadili la kusambazwa kitabu hicho linapaswa kubebwa na viongozi wa kisiasa wa Denmark. Amebainisha masikitiko yake makubwa kutokana na kuwa viongozi hao hawakuchukua hatua yoyote ya kuzuia uchapishaji wa kitabu hicho licha ya kuandikiwa barua na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiislamu na vilevile Jumuiya ya Nchi za Kiislamu wakiwataka wazuie uchapishaji wake. Katibu Mkuu wa OIC amesema katika taarifa hiyo kwamba, uchapishaji wa kitabu hicho ni hatua ya makusudi ya kueneza uadui dhidi ya Waislamu na kudhoofisha juhudi zilizofanywa na jamii ya kimataifa kwa lengo la kuimarisha maelewano na mielekeo ya kuishi pamoja kwa amani mataifa na wafuasi wa dini mbalimbali.
Taarifa hiyo imesema kuwa kuchapishwa kitabu hicho ni utumiaji mbaya wa uhuru wa kujieleza unaofanywa na baadhi ya makundi kwa shabaha ya kuzusha chuki dhidi ya Waislamu katika nchi za Magharibi.
Kitabu hicho kinachomkosea heshima Mtume Mtukufu (saw) ambacho kimepewa jina la 'Dhulma ya Kimya' kimekusanya vikatuni vyote vya kumdhalilisha Mtume vilivyochapishwa na gazeti la Denmark la Jyllands-Posten mwaka 2005. 666499