Duru ya tano ya mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi, kufasiri na kusoma Qur'ani Tukufu yanayojulikana kwa jina la Sheikh Ghanim bin Ali yamepangwa kufanyika hivi karibuni huko Doha, mji mkuu wa Qatar.
Kwa mujibu wa gazeti la as-Sharq, Khalid bin Muhammad bin Ghanim Aal Thani, mkuu wa kamati inayosimamia mashindano hayo amesema katika mkutano na waandishi habari kwamba, hatua ya kwanza ya mashindano hayo itaanza kufanyika tarehe 10 na kuendelea hadi tarehe 27 Disemba. Ameongeza kuwa hatua ya pili na ya mwisho ya mashindano hayo itaanza tarehe Mosi Januari hadi tarehe 3 mwezi huohuo. Sherehe ya kushukuru na kuwazawadia washindi wa mashindano hayo imepangwa kufanyika tarehe 13 Januari.
Amesema wanachuo wanawake na wanaume kutoka vituo vya kuhifadhi Qur'ani vinavyofungamana na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Qatar pia watashiriki katika mashindano hayo.
Usajili wa majina ya washiriki utaanza Jumatatu tarehe Mosi Novemba na kuendelea hadi trehe 11 mwezi huohuo.
Kamati inayoandaa mashindano hayo imetenga riali milioni mbili za Qatar kwa ajili ya washindi wa mashindano hayo. Waandaaji wa mashindano hayo wanasema kuwa lengo kuu ni kuwahamasisha vijana washindane katika kuhifadhi na kusoma Qur'ani kwa madhumuni ya kushikamana na maadili pamoja na mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu. 676588