IQNA

Malaysia kupeleka Pakistan nyama ya Idul Adh'ha

14:11 - November 01, 2010
Habari ID: 2023513
Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Malaysia MRCS kwa ushirikiano wa Kituo cha Utafiti na Habari za Kiislamu cha Malaysia RICOI itatekeleza hivi karibuni mpango wa kuwasaidia waathirika wa mafuriko ya Pakistan kwa kutuma nchini humo nyama ya wanyama watakaochinjwa katika siku ya Idul Adh'ha ya mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Malaysia Bernama, jumuia mbili hizo za Kiislamu zimetangaza kwamba wananchi wa Malaysia wanaweza kushiriki katika mpango huo kwa kutoa nyama ya wanyama watakaochinjwa katika siku hiyo kwa jumuiya mbili hizo ili zipate kuipeleka kwa waathirika nchini Pakistan.
Abdurahman Ismail mkuu wa Kituo cha Utafiti na Habari za Kiislamu cha Malaysia amesema kuwa watu wengine wasiokuwa Waislamu pia wanaweza kuwasaidia waathirika wa mafuriko hayo kupitia jumuia mbili hizo.
Akizungumzia suala hilo mbele ya waandishi habari, Ismail amesema kwamba anatarajia fedha nyingi zinazotumika kununulia wanyama wa kuchinjwa siku ya Idul Adh'ha zitatumika kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko ya Pakistan katika miji ya Sind na Baluchestan. Amewataka walio na hamu ya kutuma misaada yao kufanya hivyo kufikia tarehe 10 Novemba. Watu 1600 walipoteza maisha na wengine milioni moja kuwachwa bila makazi katika mafuriko hayo ambayo pia yalisababisha hasara kubwa. Watu wengine milioni 3.5 wameathirika kwa njia moja au nyingine na athari mbaya za mafuriko hayo. 685636
captcha