IQNA

Mashia kutengewa makaburi mjini Mumbai

10:25 - November 02, 2010
Habari ID: 2023747
Baada ya kufanyika juhudi kubwa za miongo miwili, hatimaye Baraza la Meya wa mji wa Mumbai nchini India limekubali ombi la Waislamu wa Kishia la kutengewa sehemu maalumu ya makaburi ya kuzikwa maiti zao.
Baraza hilo limetoa viwanja saba katika nukta tofauti za mji huo kwa lengo hilo. Kwa mujibu wa tovuti ya dnaindia, Dhul Fiqar Zeidi, mmoja wa wanachama wa Jumuiya ya Heidar ya Mumbai amezungumzia suala hilo kwa kusema kuwa Waislamu wa Kishia wamekuwa wakiishi katika mji huo kwa karibu miaka 400 sasa lakini hawajafanikiwa kutengewa sehemu maalumu ya kuzika maiti zao, na kwamba hii ndio mara ya kwanza kwao kupewa fursa hiyo. Amesema hata kama makundi mengine ya Kishia kama vile ya Mabohora wa Daudi, Mashia wa Khoja na Mashia wa Iran wamekuwa na makaburi yao maalumu, lakini Mashia wazalendo wa India walikuwa hawajawahi kupewa fursa ya kuwa na makaburi yao binafsi.
Akizungumzia jambo hilo pia, Zeinul Abedeen, mmoja wa wanachama wa Jumuiya ya Mashia wa Ithna Asheri ya Maharashtra amefurahishwa na uamuzi wa baraza hilo la mji wa kuwatengea Mashia wenyeji wa mji huo makaburi ya kuzika maiti zao baada ya juhudi za miaka mingi.
Kuna Mshia mmoja kati ya kila Waislamu watano wa mji huo, na Washia wote wakazi wa mji huo wanakisiwa kuwa kati ya watu laki tano hadi laki saba. 686595
captcha