Ihsanoglu amesema kuwa msimu wa hija ni wakati wa ibada na kumtaradhia Mola, kwa sababu hiyo zinapaswa kufanyika jitihada za kuzuia utumiaji mbaya wa anga ya kiroho ya ibada ya hija.
Katibu Mkuu wa OIC amesisitiza juu ya umoja na mshikamano wa Kiislamu kwa ajili ya kulinda anga ya kiroho ya hija na akasema kuwa kwa sasa ulimwengu wa Kiislamu unapitia katika moja ya vipindi vyenye mivutano mikubwa zaidi katika historia na makundi mbalimbali ya Kiislamu yanapaswa kuungana kwa ajili ya kukabiliana na mivutano hiyo.
Vilevile Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu amewataka viongozi na nchi za Kiislamu kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na changamoto za kidini, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kijamii na kielimu.
Ihsanoglu ameashiria marekebisho yaliyofanyika katika jumuiya ya OIC miaka sita iliyopita na akasema kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu imekuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na hali hiyo ngumu. 691466