Suala la Cyprus Kaskazini inayodhibitiwa na Waturuki kupata uanachama wa kudumu katika Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC lilijadiliwa kwa kina siku ya Jumapili kati ya viongozi wa jamhuri hiyo na Mahmut Erol Kılıç, Katibu Mkuu wa Muungano wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu.
Mahmut Erol Kılıç ambaye amekuwa katika jamhuri hiyo ya Cyprus Kaskazini kwa madhumuni ya kushiriki katika shehere za kuadhimishwa mwaka wa 27 wa uhuru wake amesema katika mazungumzo yake na Rais Derviş Eroğlu wa jamhuri hiyo kwamba suala la uanachama wa Cyprus Kaskazini hiyo katika OIC litatatuliwa hivi karibuni.
Mahmut Erol Kılıç amesema kuwa atatumia nafasi yake ya ukatibu mkuu katika Muungano wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu kuzishawishi nchi hizo zikubali uanachama wa kudumu wa Jamhuri ya Cyprus Kaskazini ambayo hivi sasa ni mwanachama mtazamaji tu katika muungano huo.
Jamhuri ya Cyprus Kaskazini ilijitangazia uhuru wake mwaka 1983. 695857