IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Saudia kufanyika mwezi ujao

17:54 - November 22, 2010
Habari ID: 2036102
Mashindano ya 32 ya Kimataifa ya kuhifadhi, kusoma na kufasiri Qur'ani Tukufu ya Saudi Arabia yataanza tarehe 27 Disemba katika mji mtakatifu wa Makka.
Mkurugenzi wa mashindano hayo Mansur bin Muhammad al Samiih amesema kuwa mashindano hayo yatafanyika katika awamu tano za kuhifadhi Qur'ani kamili pamoja na tajdwidi na tafsiri ya maana za kitabu hicho, kuhifadhi Qur'ani kamili pamoja na tajwidi na qiraa, kuhifadhi juzuu 20 pamoja na tajwidi na qiraa, kuhifadhi juzuu 10 pamoja na tajwidi na qiraa, kuhifadhi juzuu 5 pamoja na tajwidi na qiraa makhususi kwa wawakilishi wa jumuiya za Kiislamu kutoka nchi zisizokuwa za Waislamu.
Ameongeza kuwa washiriki 122 kutoka nchi 38 duniani na washiriki wengine 66 kutoka jumuiya 26 za Kiislamu za nchi zisizokuwa za Waislamu watashiriki katika mashindano hayo. Mansur bin Muhammad al Samiih amesema kuwa majaji 10 kutoka nchi za Saudia, Misri, Syria, Morocco, Nigeria, Indonesia na Brunei watasimamia mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani.
Mkurugenzi wa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Saudi Arabia amesema kuwa mashindano hayo yanasimamiwa na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Saudi Arabia. 699829
captcha