IQNA

Sisitizo la OIC juu ya kuunga mkono taifa la Palestina

13:01 - December 01, 2010
Habari ID: 2040714
Fuad Maznai, mkuu wa ujumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ambao umeutembelea Ukanda wa Gaza amesisitiza juu ya nafasi ya jumuiya hiyo katika kuunga mkono taifa dhulumiwa la Palestina
Kwa mujibu wa tovuti ya jumuiya hiyo, Maznai ambaye anasimamia kitengo cha masuala ya kibinadamu cha OIC ameashiria msimamo imara wa jumuiya hiyo pamoja na wa katibu mkuu wake Ekmeleddin Ihsanoghlu, wa kutafuta uungaji mkono wa kimataifa kwa maslahi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Maznai amebainisha malengo ya safari ya ujumbe huo uliojumuisha timu ya madaktari 16 na wawakilishi wa nchi kadhaa za Kiislamu wanachama wa OIC katika Ukanda wa Gaza na kusema kwamba, moja ya malengo hayo ni kutekeleza maagizo ya Katibu Mkuu wa OIC kuhusiana na maamuzi yaliyochukuliwa na mawaziri wa OIC kuhusu ukanda huo. Ameongeza kuwa malengo mengine yamekuwa ni kuchunguza hali ya kimaisha ya wakazi wa eneo hilo na hasa kuhusu suala la afya, kunufaika na ushirikiano wa nchi wanachama wa OIC kwa maslahi ya wananchi wa Palestina, kuzinduliwa miradi muhimu na ya kimsingi iliyodhaminiwa na nchi wanachama, kurudisha shukrani kwa juhudi za baadhi ya nchi za Kiislamu za kuwasaidia kwa hali na mali Wapalestina na pia kutumwa katika ukanda huo timu ya madaktari na wataalamu kwa ajili ya kutekeleza huko ratiba maalumu ya kitiba.
Mwishoni Maznai ameashiria ombi la Katibu Mkuu wa OIC kwa nchi za Kiislamu la kuzitaka zifanye kila liwezekanalo kwa ajili ya kupunguza machungu ya wananchi wa Palestina na hasa wa Ukanda wa Gaza.
Hivi sasa asilimia 80 ya wananchi hao wanaishi chini ya mstari wa umasikini. Watoto waliowengi wa ukanda huo wanakabiliwa na matatizo mengi ya kisaokolojia na kinafsi yanayotokana na vikwazo na athari za vita. 704611
captcha