IQNA

Mashindano ya kimataifa ya kuandika makala ya Tuzo ya Kimataifa ya Imam Ali (as)

19:26 - December 06, 2010
Habari ID: 2043397
Mashindano ya Tuzo ya Kimataifa ya Imam Ali (as) ya kuandika makala kuhusu shakhsia huyo na sira yake katika zama zilizopita, kipindi cha sasa na mustakbali yamepangwa kufanyika hivi karibuni.
Mwenyekiti wa kamati andalizi ya mashindano hayo Ali Jihad amesema kuwa mashindano hayo ya kimataifa yatafanyika kwa mnasaba wa kuchaguliwa mji mtakatifu wa Najaf kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu katika maka 2012. Wanafikra na watafiti wanaalikwa kutuma makala zao za kifikra kwa uongozi wa haram ya Imam Ali bin Abi Twalib mjini Najaf nchini Iraq.
Ali Jihad amesema kuwa mashindano hayo yanafanyika kwa lengo la kusisitiza juu ya utambulisho wa kimataifa wa Uislamu, kuimarisha uhusiano kati ya tamaduni mbalimbali kupitia njia ya uhakiki na uchunguzi katika masuala ya kibinadamu yaliyohuishwa na Imam Ali bin Abi Twalib kielimu na kivitendo.
Ameongeza kuwa malengo mengine ya mashindano hayo ya kimataifa ni kubainisha upande wa maarifa, mwenendo na shakhsia ya Imam Ali (as), kutambua ulimwengu mpya kupitia shakhsia ya Amirul Muuminin (as) na kadhalika.
Amesema kuwa haram ya Imam Ali (as) itatoa zawadi ya nishani ya dhahabu na dola elfu kumi kwa mshindi wa kwanza na nishani ya fedha na dola 7500 kwa mshindi wa pili. 707379

captcha